Skip to main content

Ban anahisi kuna changamoto kabla ya kukamilika amani Sudan

Ban anahisi kuna changamoto kabla ya kukamilika amani Sudan

Mwaka huu wa mwisho wa utekelezaji wa makubaliano ya amani ya 2005 yaliyotiwa saini kati ya kundi la ukombozi wa Sudan SPLA na serikali ya Sudan, utakua mgumu sana, amesema katibu mkuu wa UM Ban Ki-moon.

Katika taarifa yake kuadhimisha mwaka wa tano tangu kufikiwa makubaliano ya amani siku ya Jumapili, katibu mkuu alisema changamoto kuu itakua wakati pande zote zinapojitayarisha kuanda uchaguzi mkuu na kura ya maoni ya kujiamulia uhuru kwa wakazi wa Sudan ya Kusini. Makubaliano yalimaliza zaidi ya miaka 20 ya vita kati ya kaskazini na kusini. Bw Ban amesema changamoto zilizopo zitahitaji pande zote zinazohusika kubuni kwa haraka kabisa mfumo wa kisheria, kisiasa na taasisi za kuendesha uchaguzi wa huru, haki na kuaminika. Katibu mkuu hata hivyo alisema, maendeleo muhimu yamepatikana mnamo miaka mitano iliyopita na kuhimiza kila upande kuongeza mara mbili juhudi zao kuelekea upatanishi.