Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mvua kali zasababisha maelfu ya watu kuathirika Kenya

Mvua kali zasababisha maelfu ya watu kuathirika Kenya

Afisa wa idara ya umoja wa mataifa juu ya Misaada ya Dharura (OCHA), Bi Elisabeth Byrs amesema kati ya Disemba 27 mwaka 2009 hadi Januari 5 2010 kumekuwepo na mvua kali huko maeneo ya Kaskazini, Kati na Magharibi mwa Kenya , na kuwathiri watu elfu 30.

Shirika la msalaba mwekundu huko Kenya liliripoti kwamba watu 21 wamefariki hadi hivi sasa kutokana na mafuriko, lakini idadi hiyo haijathibitishwa bado. Maeneo yaliyoathirika zaidi ni Turkana huko kaskazini ya Kenya, ambako watu elfu 20 wameathirika na elfu 10 wamepoteza makazi yao.

Kumekuwepo na uharibifu mkubwa upande wa miundo mbinu hasa majengo ya shule, barabara na huduma za maji, pamoja na vijiji vingi kutoweza kupokea misaada na vifaa kutokana na kuharibika njia zote za mawasiliano. Wakazi wengi ambao waliweza kufika katika kambi huko Naivasha kati kati ya Kenya wanamahitaji makubwa ya msaada wa dharura. OCHA imekua inashiriki katika tume ya pamoja ya kuthatmini hali ya mambo pamoja na shirika la watoto la umoja wa mataifa na serekali ya Kenya. Na kama inavyotarajiwa wasi wasi mkubwa kabisa wa OCHA kutokana na mafuriko ni kuzuka kwa magonjwa hasa kipindupindu, na kuna mahitaji ya dharura ya maji masafi. Shirika la msalaba mwekundi linahitaji pia akiba zaidi ya dawa za kupambana na kipindupindu.

Bi Byrs anasema ingawa msimu wa mvua Kenya ulitarajiwa wakati huu lakini mvua zimekua kubwa kuliko kawaida yake.

"Mvua hizi si za kawaida, ni majira ya mvua lakini mvua zimekua nyingi kuliko ilivyo kawaida yake. Kwa hakika ni hali mbaya sana na mvua hizo zote zimesababisha mafuriko makubwa, mito imefurika kupindukia ukingo na hivyo kusababisha mafuriko kwenye vijiji vingi hasa katika majimbo matatu makuu ya Kenya. Kuhusiana na makambi, ambayo nina habari nazo ni yale yanayopatikana katikati ya Naivasha ambako kuna watu elfu 5 walipoteza makazi yao wanaoishi ndani ya hema. Kunahaja ya kuimarisha hali ya kusikitisha wanaoishi watu katika makambi kwa wakati huu."