WFP imesitisha msaada Kusini mwa Somalia
Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limesema vitisho vya kundi la wanamgambo al Shaabab linalodhibiti asimilia 95 ya eneo la kusini mwa Somalia limeathiri shughuli zake za misaada.
WFP imesema kundi hilo la wanamgambo wenye silaha limekuwa likidai takribani dola za Kimarekani elfu 20,000 kila kipindi cha miezi sita kwa ajili ya masuala ya ulinzi na kuwafuta kazi wanawake. Kwa mujibu wa msemaji wa WFP mjini Geneva Emilia Casella madai ya wanamgambo hayakubaliki . Amesema shirika hilo linafunga ofisi zake sita katika eneo hilo na kuondosha wafanyakazi wake, msaada wa chakula na vifaa kupeleka katika maeneo mengine yenye usalama nchini humo.
"Kimsingi athari ni kwamba watu wapatao milioni moja waliokuwa wakiishi kwa kutegemea msaada wa chakula kusini mwa Somalia wanakabiliwa na hali mbaya , wengi wao wanategemea sana msaada wa chakula na kwa bahati mbaya kwa wakati huu hatutaweza kuwapatia msaada huo wa chakula. Tunahofia sana madhara yake hususan kwa watoto na wanawake. Tutaendelea kuangalia uwezekano wa kurejesha shughuli zetu katika hali ya kawaida haraka iwezekanavyo, lakini kwa kweli dhamana ni juu ya wanaodhibiti eneo hilo kuheshimu misingi ya kibinadamu na kuhakikisha kwamba wafanyakazi wa nje wanakuwa na usalama wa kutosha na wanaweza kufanya kazi yao."
WFP hata hivyo imesema itaendelea kutoa msaada wa chakula kwa maeneo mengine ya Somalia ikiwa ni pamoja na mji mkuu Mogadishu kwa lengo la kuwafikia watu takribani milioni moja nukta nane.