Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu anasema "kashtushwa" na miripuko ya ghasia katika Iran

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu anasema "kashtushwa" na miripuko ya ghasia katika Iran

Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu kwenye taarifa aliotoa kwa vyombo vya habari Ijumatano alisema ya kuwa alishtushwa na kile alichokiita "mfumko wa vifo, majeraha na watu kukamatwa" katika Jamhuri ya KiIslam ya Iran.

Alisema licha ya kuwa "hakuna taarifa hakika" zenye kuelezea "hali halisi iliyosababisha vifo vinavyokadiriwa watu saba, na idadi kadha ya majeruhi, wakati wa taadhima za kuihishimu Sikukuu ya Ashoura, mnamo Ijumapili iliopita" taarifa zilizopokewa na Pillay kwa hivi sasa, zilieleza "vikosi vya usalama pamoja na wanamgambo wa Iran wa Basij wenye hadhi ya kijeshi, walitumia nguvu iliokiuka kawaida" dhidi ya raia. Alisisitiza kwamba ni wajibu wa Serikali ya Jamhuri ya KiIslam ya Iran kuhakikisha "fujo na vurugu huwa zinadhibitiwa na hazitoenea zaidi nchini." Alisema raia wana haki ya "kuelezea hisia zao hadharani, na kuandamana kwa utulivu bila ya kupigwa wala kuchapwa marungu au kutupwa gerezani na watumishi wa idara ya usalama." Alisihi raia waliokamatwa na kuwekwa gerezani, kwa sababu zo zote zile, wanawajibika kufanyiwa kesi na haki ya kutetewa, kwa kulingana na kanuni za kimataifa juu ya haki za binadamu, ikijumlisha pia ule Mkataba wa Kimataifa juu ya Haki za Kiraia na Kisiasa."