Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID/Sudan waahidi ushirikiano kuimarisha usalama Darfur

UNAMID/Sudan waahidi ushirikiano kuimarisha usalama Darfur

Wawakilishi wa Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) pamoja na wawakilishi wa Serikali ya Sudan wameripotiwa kutiliana sahihi makubaliano ya jumla, kuhusu mradi wa utendaji, uliokusudiwa kuhakikisha watumishi wa UNAMID pamoja na mali zao, huwa watapatiwa usalama wanaostahiki kwenye jimbo la mvutano la Sudan Magharibi la Darfur.

 Kwa mujibu wa taarifa ya Liuteni-Jenerali Patrick Nyamvumba, Kamanda Mkuu wa Vikosi vya UNAMID itifaki yao hii itasaidia kuimarisha zaidi mapatano yaliopo kwa sasa hivi, kuhusu Hadhi-ya-Sheria-ya-Vikosi vya UNAMID (SOFA), kanuni ambayo, alitilia mkazo, itawapatia "hatua ziada za kusitisha na kuzuia vitendo vinavyosababisha mazingira yasio salama katika Darfur, hali ambayo ilionekana kuendelea kupanuka katika miezi ya karibuni." Utiaji sahihi mapatano haya ulifanyika kufuatilia kikao cha utendaji kazi, kilichokutana Khartoum Ijumapili, tarehe 20 Disemba 2009, ambapo wawakilishi wa UNAMID na Serikali walizingatia uwezo na njia za kuchukuliwa pamoja, kupunguza mashambulio dhidi ya wafanyakazi wa UNAMID.