Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuzorotwa kwa suluhu Ghaza, mwaka mmoja baada ya mapambano, kwahatarisha maisha ya umma, anasema KM

Kuzorotwa kwa suluhu Ghaza, mwaka mmoja baada ya mapambano, kwahatarisha maisha ya umma, anasema KM

Tarehe ya leo, inakamilisha mwaka mmoja tangu majeshi ya Israel yalipovamia eneo la WaFalastina la Tarafa ya Ghaza, mnamo Disemba 27 mwaka 2008, ambapo kwa wiki tatu kuliendelezwa operesheni za kijeshi zilizopewa jina la "Operesheni ya Kumwaga Risasi".

Kwenye mashambulio haya ya vikosi vya Israel, watu 1,400 ziada waliuawa kwenye eneo la Ghaza, na watu 5,000 wengine walijeruhiwa na majumba, maskuli, hospitali pamoja na marikiti kadha ziliangamizwa na kugeuzwa vifusi na kokoto. Waisraili walidai walilazimika kuvamia Ghaza ili kukomesha mashambulio ya makombora ya kienyeji, yaliokuwa yakirushwa na wapambanaji wa KiFalastina kutokea Ghaza. Risala ya KM Ban Ki-moon, ya kumbukumbu ya kutimia mwaka mmoja ya uvamizi wa Tarafa ya Ghaza na majeshi ya Israel, inalezea wasiwasi wake mkuu kwamba hadi sasa yale masuala yaliochochea mapigano na matokeo yaliofuatia, yenye wahaka mkubwa kwa maisha ya wakazi wa Ghaza na jamii za huko, bado hayajashughulikiwa wala kuzingatiwa kama inavyotakikana. Taarifa hiyo iliotolewa na Msemaji wa KM ilisisitiza "ni masuala machache tu muhimu, yaliopendekezwa na azimio la Baraza la Usalama 1860, yanayotakikana kutekelezwa kidharura, yaliweza kutimizwa." Alisema viwango vya bidhaa zinazoruhusiwa kuingizwa kwenye Ghaza, pamoja na ubora wa vitu hivyo haukuridhisha hata kidogo. Taarifa ya KM ilisisitiza pia ya kuwa "shughuli za kiuchumi, kwa ujumla, zimezirai na kuzorota, pamoja na harakati za ujenzi wa majumba yalioangamizwa na mashambulio ya Israel, na umma wa Ghaza unanyimwa vile vile haki za kimsingi za kibinadamu." Alisisitiza kwamba kunahitajika mwelekeo mpya kabisa, wa dharura, kukabili hali duni iliolivaa eneo la Tarafa ya Ghaza. Aliitaka Israel ikomeshe, haraka, vikwazo visiokubalika dhidi ya Ghaza ambavyo havisaidii kuharakisha ufufuaji wa shughuli za kiuchumi na zakiraia kwenye eneo. Wkati huo huo KM alililiomba kundi la WaFalastina la Hmas kusitisha vitendo vya kutumia nguvu na kuhishimu kikamilifu sheria ya kimataifa