Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK), na pia Mkuu wa Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) leo alichapisha kwenye gazeti la kila siku la Marekani, linaloitwa The Washington Times, insha yenye maelezo maalumu yaliokumbusha mchango wa kila siku wa UM, katika kuwatekelezea maelfu ya raia haki zao za kimsingi, kwenye mazingira ya

wasiwasi katika eneo hilo la Maziwa Makuu. Taarifa ya Doss ilikusudiwa kujibu ripoti ya kundi linalotetea haki za binadamu la Human Rights Watch, yenye madai kwamba vikosi vya UM katika JKK, vilishirikiana na wanajeshi wa taifa wa FARDC, ambao baadhi ya askari wao walituhumiwa "kutenda ukatili uliokiuka mipaka, dhidi ya raia" wakati walipokuwa wakiendeleza operesheni za kuwasaka waasi waliojificha kwenye maeneo kadha ya nchi. Kama inavyokumbukwa, wiki iliopita Baraza la Usalama lilitoa mwito uliosisitiza, kwa mara nyengine tena, kwamba majeshi ya MONUC, yanawajibika kutumia "njia zote ziliopo za kijeshi" kuhami raia ambao maisha yao huhatarishwa na makundi ya aina yoyote katika JKK. Mwito huu wa Baraza la Usalama ulitolewa baada ya kupokewa ripoti zilizobainisha kufanyika mauaji ya halaiki ya raia, na ukiukaji wa haki za binadamu ulioendelezwa na wanajeshi wa Serikali na waasi, hasa kwenye maeneo ya uhasama ya mashariki. Makala ya Doss ilisema vikosi vya MONUC viliidhinishwa na Baraza la Usalama kulisaidia jeshi la taifa la FARDC kupatiwa huduma za kilojistiki katika operesheni za kushambulia waasi na kuwang'oa kutoka yale maeneo waliokuwa wamejizatiti kutishia raia, na kuhakikisha hawatorejea tena kwenye sehemu hizi za nchi.


Shirika la Kimataifa Juu ya Usafiri Salama wa Ndege za Kiraia (ICAO), limeamua kuharakisha utekelezaji wa ule mradi wa utendaji wa kuzuia na kudhibiti bora utoaji wa gesi chafu zinazoongeza halijoto ulimwenguni, licha ya kuwa kwenye Mkutano wa Copenhagen wa COP15, uliomalizika karibuni, mataifa hayajapitisha itifaki ya viwango vinavyoruhusiwa kumwagwa kwenye anga na vyombo vya anga na vile vya baharini. Kwenye mkutano wa hadhi ya juu wa ICAO, uliofanyika mwezi Oktoba 2000, nchi zinazowakilisha asilimia 93 ya misafara ya ndege za kiraia duniani, zilikubaliana kupunguza athari za safari za ndege kwenye hali ya hewa, na kuweka lengo la kudhibiti kwa asilimia 2, kila mwaka, yale matumizi ya mafuta ya ndege, mpaka 2050 ili, hatimaye, kusawazisha viwango vya gesi chafu inayotolewa kwenye anga na ndege. Mataifa Wanachama wa ICAO, wakichanganyika na juhudi zilizoendelezwa na viwanda vya usafiri wa anga, kwa miaka mingi waliweza kuchukua hatua zilizofaa kupunguza athari ya kwenye mazingira iliochochewa na usafiri wa ndege. Haya ni mapatano ya awali, kimataifa, yaliokabili kipamoja udhibiti wa mabadiliko ya hali ya hewa kutokana na sekta moja maalumu ya kiuchumi.