Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

BU lapitisha azimio kuidhinisha MONUC kutumia "nyenzo zote za lazima" kuwahami raia katika JKK

BU lapitisha azimio kuidhinisha MONUC kutumia "nyenzo zote za lazima" kuwahami raia katika JKK

Ijumatano wajumbe wa Baraza la Usalama (BU), wanaowakilisha mataifa wanachama 15, walipitisha, kwa kauli moja, azimio lenye kuruhusu Vikosi vya Ulinzi Amani vya UM katika JKK (MONUC), kutumia "uwezo wote walionao", chini ya Mlango wa VII wa Mkataba wa UM, unaoruhusu kutumia nguvu, ili kuwapatia raia hifadhi wanayostahiki, dhidi ya mashambulio kutoka makundi yote yenye kuhatarisha usalama wao.

Azimio lilitilia mkazo kwamba vikosi vya MONUC vinaipa umuhimu mkubwa kabisa ile kadhia ya kuvisaidia vikosi vya taifa katika JKK, vinavyojulikana kama vikosi vya FARDC, kupata lojistiki na vifaa vya kuwazuia waasi wasirejee tena kwenye yale maeneo waliokuwa wakiyakalia kimabavu katika siku za nyuma. Azimio la Baraza la Usalama, limeidhinisha operesheni za vikosi vya MONUC katika JKK, vinavyojumlisha wanajeshi pamoja na polisi wa kimataifa 22,000, ziendelee nchini mpaka tarehe 31 Mei 2010, ambapo huduma hizo huenda zikaongezwa tena kwa miezi 12 ziada, kwa kutegemea hali ya usalama ilivyo huko kwa wakati huo.