Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa misaada ya dharura ahimiza hifadhi bora kwa raia wa JKK dhidi ya mashambulio ya waasi wa LRA

Mkuu wa misaada ya dharura ahimiza hifadhi bora kwa raia wa JKK dhidi ya mashambulio ya waasi wa LRA

John Holmes, Naibu KM juu ya Masuala ya Kiutu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, ametoa mwito maalumu unaopendekeza jamii ya kimataifa ichukue hatua za nguvu zaidi zitakazohakikisha raia wanaokabiliwa na hatari ya kushambuliwa na waasi wa Uganda, wa kundi la LRA, huwa wanapatiwa ulinzi na hifadhi inayofaa kuwanusuru kimaisha.

Mwito huu ulitolewa hii leo, kwa kuambatana na siku ya ukumbusho wa mauaji ya halaiki ya raia wa JKK yalioendelezwa na waasi wa kundi la LRA, mnamo Siku ya Krismasi ya 2008. Kwa mujibu wa ripoti za UM, baina ya tarehe 25 mpaka 27 Disemba 2008, waasi wa LRA, walifanya shambulio katili kwenye kanisa na katika vijiji vya mbali vya maeneo ya Dungu na Doruma, kwenye wilaya ya Haut Uele, iliopo katika Jimbo la Orientale kaskazini, katika JKK. Kwenye shambulio hili, waasi waliuwa raia 400 ziada. Kadhalika ripoti za karibuni za UM, ambazo bado hazijathibitishwa, zinaeleza kwamba baina ya tarehe 14 mpaka 20 Disemba, mwaka huu, makundi ya LRA yalifanya mashambulio matatu katika JKK yaliosababisha watu 47 kuuawa. Holmes alisisitiza hatari ya vitisho vya waasi wa LRA inakabili eneo zima la Maziwa Makuu na kunatakikana juhudi na bidii za serikali ya JKK na zile za nchi jirani, zikichanganyika na jamii ya kimataifa kulitaua suluhu hili kwa mara ya mwisho lisiibuke tena kieneo.