Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa BK asema karidhika na shughuli za kikao cha 2009

Rais wa BK asema karidhika na shughuli za kikao cha 2009

Ali Abdussalam Treki wa Libya, Raisi wa kikao cha 2009 cha Baraza Kuu (BK) la UM - kikao cha 64 - Ijumanne adhuhuri, alikuwa na mahojiano ya kufunga mwaka, na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu.

Raisi wa bodi hili la UM, lenye wanachama 192, alieleza ya kuwa kwenye mikutano 66 ya Baraza Kuu, iliofanyika tangu kikao cha 64 kuanza mwezi Septemba, kulipitishwa maazimio 226 pamoja na kufanyika maamuzi 57. Alisema hivi sasa Baraza linakaribia kukamilisha ratiba ya kazi kwa robo ya kwanza, ambapo kamati tano, kati ya Kamati Kuu sita za Baraza Kuu, zimeshakamilisha shughuli zao, isipokuwa Kamati ya Tano, inayoshughulika na Bajeti na Utawala, inayotazamiwa kumaliza kazi wiki hii. Vile vile, alikumbusha kwamba mikutano muhimu mitatu ya Baraza Kuu ilifanyika nje ya Makao Makuu, mwaka huu, ikijumlisha Mkutano Mkuu wa Roma, Utaliana juu ya Dhamana ya Akiba ya Chakula Maridhawa kwa wote, kikao cha Nairobi, Kenya kilichozungumzia Ushirikiano wa Kimaendeleo kwa Mataifa ya Kizio cha Kusini ya Dunia, na Mkutano Mkuu wa UM juu ya Udhibiti wa Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa uliofanyika kwenye mji wa Copenhagen, Denmark na uliomalizika mwisho wa wiki iliopita. Balozi Treki alieleza mwakani Baraza Kuu litaendelea kulenga shughuli zake kwenye masuala kadha yanayotatanisha ulimwengu - kuanzia juhudi za kuimarisha huduma za maendeleo, kusawazisha utulivu na amani ya kimataifa, na vile vile kwenye utekelezaji wa haki za binadamu kwa wote. Alikumbusha Raisi Treki juu ya kufanyika Mkutano Mkuu wa Vyeo vya Juu, mwakani, kuzingatia taratibu za pamoja, zinazotakikana kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia, ya kupunguza ufukara na hali duni kabla ya 2015. Kuhusu suala la kuleta mageuzi kwenye UM na taasisi zake, yatakayolingana na wakati, Balozi Treki alisema Baraza linaendelea kusailia njia za kujirekibisha, na vile vile alisema kikao cha awali, juu ya kuleta mageuzi katika Baraza la Usalama kimeshafanyika mwaka huu, na wajumbe wa kimataifa wanajiandaa, sasa hivi, kushiriki kwenye duru ya pili, mapema 2010, kuendelea na mazungumzo kuhusu marekibisho ya katika Baraza la Usalama.