Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Mashirika ya UM yanayohudumia misaada ya kiutu wiki hii yameanza kufarajia vifaa vya kunusuru maisha katika Malawi kaskazini, kufuatia mitetemeko ya ardhi iliopiga huko mwezi huu na kuua watu wanne, kujeruhi watu 300 ziada na kuharibu au kubomoa nyumba karibu 4,000. Wilaya ya Karonga, Malawi kaskazini iliathirika vibaya zaidi kufuatia msururu wa zilzala zilizopiga kuanzia tarehe 06 mpaka 20 Disemba, mitetemeko iliokadiriwa kuvuka vipimo vya baina ya 5.4 na 6.0 Richter, kwa mujibu wa taarifa ya Shrika la UM juuya Misaada ya Dharura (OCHA). Tume ya kiufundi ya pamoja, ikijumuisha watumishi wa shirika la UM juu ya maendeleo ya watoto, UNICEF; miradi ya chakula, WFP; huduma za chakula na kilimo, FAO, pamoja na taasisi juu ya udhibiti wa watu, UNFPA Ijumatano walielekea Karonga kufanya tathmini halisi juu ya mahitaji ya kiutu, hasa yale yanayohusu afya na lishe, maji salama, usafi, vifaa vya ilmu na akiba ya chakula. Mashirika ya UM yanayohudumia misaada ya kiutu yameeleza kushirikiana, kwa ukaribu zaidi, na mashirika yasio ya kiserikali pamoja maofisa wa Seikali ya Malawi katika kusimamia huduma za kufarajia waathirika wa mitetemeko ya ardhi nchini.