Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlinzi wa majengo ya UM Usomali auawa

Mlinzi wa majengo ya UM Usomali auawa

UM imeripoti Ijumanne majambazi kadha walimpiga risasi na kumwua ofisa raia wa usalama nchini Usomali, aliyekuwa akitumikia Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP), kitendo kilichotukia kwenye mji wa Beledweyn, Usomali.

Ofisa mlinzi huyo, anayeitwa Ali Farah Amey, alikuwa mkuu wa askari walinzi wa majengo ya ofisi za UM ziliopo karibu na mpaka wa Ethiopia, kilomita 300 (maili 180) kaskakzini ya mji mkuu wa Usomali wa Mogadishu. Kwa mujibu wa taarifa kwa waandishi habari, kutoka mtumishi mmoja mwenyeji, anayefanya kazi na UM, aliyeshuhudia tukio hilo, alieleza kwamba majambazi "walimdunga risasi (Ali Farah Amey), mara chache kwenye kichwa na mabega, na alifariki papo hapo" baada ya shambulio. Marehemu alikuwa akinywa chai mkahawani alipovamiwa na watu wasiotambulikana. Mashirika ya UM yanayohudumia misaada ya kiutu katika Usomali, pamoja na mashirika wenzi, yasio ya kiserikali, yaliopo Usomali, yanaendelea kusumbuliwa na vitisho vya mara kwa mara, kutoka majambazi, vitisho ambavyo hukwamisha uwezo wa mashirika ya kimataifa, kufarajia huduma za kiutu kwa umma muhitaji unaoishi katika maeneo yaliozingwa na miripuko ya mapigano na uhasama katika Usomali.