Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Terje Roed-Larsen, mjumbe wa UM anayehusika na utekelezaji wa Azimio 1559 (2004) la Baraza la Usalama, ameripotiwa na Msemaji wa KM, Martin Nesirky, kwamba huwa anashauriana mara kwa mara na maofisa wa Lebanon kadha pamoja na washirika wengine wa Ki-Arabu katika eneo, na vile huwa anashauriana na mataifa yote mengine yanayohusika na utekelezaji wa azimio hilo la Baraza la Usalama. Taarifa hii ilitolewa kujibu suala kujua nani hushirikiana na mjumbe wa UM juu ya utekelezaji wa Azimio husika. Azimio 1559 la Baraza la Usalama lilipopitishwa 2004 lilikusudiwa hasa kuunga mkono pendekezo la kufanyisha uchaguzi wa uraisi Lebanon, ulio huru na wa haki; na lilitilia mkazo kuondoshwa kwa “vikosi vya kigeni” viliopo Lebanon, kwa wakati huo, ikimaanisha, kwa lugha ya kidiplomasiya, vikosi vya Syria. Kwa hivi sasa Syria imekataa kabisa kujihusisha, wala kushiriki kwenye mashauriano ya aina yoyote yale yanayosimamiwa na mjumbe wa UM, Terje Roed-Larsen.

Gay McDougall, Mtaalamu Huru wa UM juu ya masuala ya makundi yalio wachache, ameiomba Serikali ya Uchina kuruhusu kufanyika tathmini ya jumla, na inayojitegemea, kutathminia, mapema iwezekanavyo, mvutano wa kikabila uliosababisha fujo na vurugu kuripuka kwenye mji wa Urumqi, katika Jimbo Linalojitawala la Uyghur, mnamo Julai 2009. McDougall alieleza kwamba "uchanganuzi makinifu wa matukio hayo unahitajika kuendelezwa kwa lengo la kugundua kiini halisi cha mvutano wa kikabila, uliosababisha msiba wa kutisha na upotezaji maisha ulioshuhudiwa na jamii za makabila yote mawili yanayoishi kwenye Jimbo la Uighur."

Kadhalika, Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) katika mwisho wa wiki iliopita, lilitangaza taarifa maalumu kwa waandishi habari, ilioeleza UM kuingiwa wasiwasi mkuu juu ya uamuzi wa wenye madaraka Cambodia, wa kuwarudisha kwa nguvu Uchina, Wa-Uighurs 20 waliopeleka maombi ya kutaka hifadhi ya siasa. Kwa mujibu wa taarifa za UNHCR Wa-Uighurs hawa kisheria hawawezi kurejeshwa Uchina, kwa sababu kesi yao bado haijazingatiwa wala kusikilizwa na wenye madaraka Cambodia. UNHCR ilihadharisha kwamba mwelekeo wa maamuzi kama haya, usioridhisha, unaonekana kushika mizizi kwa wingi katika kipindi cha karibuni, takriban, katika sehemu nyingi za dunia, kinyume na kanuni za kimataifa. Taarifa ya UNHCR ilikumbusha kwamba mataifa yote huwajibika, na kulazimika, kwa uwiano na sheria ya kimataifa juu ya haki za wahamiaji, "kutomrejesha nchini kwao, mhamiaji aanayeomba hifadhi ya kisiasa, bila ya kuzingatia maombi yake, na hasa ikiwa mhamiaji huyo huwa anakhofia atakaporejeshwa kwao atateswa na kuadhibiwa" na wenye madaraka. Ijumaa iliopita UNHCR iliitumia Serikali ya Kifalme ya Cambodia ombi maalumu la kupendekeza ipatiwe maelezo kamili juu ya kesi ya Wa-Uighurs 20 waliondoshwa nchini kimabavu, na kupelekwa Uchina, bila ya idhini yao, kitendo ambacho tumearifiwa kimeharamisha haki za kimsingi za kimataifa juu ya wahamiaji.