Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM imelaumu vikali waasi wa LRA kwa mauaji na mateso ya raia katika JKK

UM imelaumu vikali waasi wa LRA kwa mauaji na mateso ya raia katika JKK

Vile vile hii leo, kumewasilishwa ripoti nyengine ya apmoja ya Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu (OHCHR) na Shirika la Ulinzi Amani la UM katika JKK (MONUC) kuhusu mashambulio ya kikatili yaliofanywa na waasi wa LRA katika JKK.

 Kwa mujibu wa ripoti, mnamo kipindi cha kuanzia Septemba 2008 hadi mwezi Juni 2009, baada waasi wa LRA kuendeleza darzeni za mashambulio kwenye miji na vijiji viliopo jimbo la Orientale la JKK, waliripotiwa kuuwa raia 1,200, pamoja na kuteka nyara watu 1,400 na kuwang'oa makazi kimabavu watu 230,000, hujuma ambazo zilijumlisha vitendo karaha vya kukata viungo raia, kutesa na kunajisi wanawake kihorera. Ripoti ilithibitisha pia kwamba mara nyingi wanawake na watoto wa kike wanaonajisiwa kimabavu na waasi wa LRA huuawa baadaye, na wingi wa wanawake waliotoroshwa "hulazimishwa kuolewa na wafuasi wa LRA na kufanywa watumwa wa kijinsia, halkadhalika." Raia waliosaidia kuwazika maiti walionajisiwa na waasi, karibuni walitoa ushahidi, kwa kiapo, kwa wachunguzi wa UM wa haki za binadamu, kwenye mji wa Batande, ambapo walithibitisha ya kuwa walishuhudia darzeni moja ya maiti wa kike walionajisiwa na waasi, mabibi ambao "walifungwa mikono nyuma, kanzu zao zilichanwa na miguu kupanuliwa." Ripoti imependekeza kwa jamii ya kimataifa, hasa serikali za eneo, kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) na kuwasaka viongozi wa LRA, kuwakamata na kuwakabidhi Mahakama ya ICC kukabili haki.