Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Msafara wa Shirika la UM juu ya Amani katika Jamhuri ya AfrIka ya Kati na Chad (MINURCAT), unaohusika na ugawaji wa vitu na watu, uliojumuisha magari ya kiraia matatu, ulishambuliwa Ijumapili na watu wanne wasiotambulika waliochukua silaha, kwenye eneo la kusini-mashariki katika Chad. Vikosi vya MINURCAT vilipelekwa haraka kwenye eneo, pamoja na wahudumia tiba ili kuokoa watumishi waliopatwa na ajali hiyo, pamoja na kuyaokoa magari ya MINURACT yalioharibiwa na mashambulio.

KM alipokutana asubuhi na waandishi habari wa kimataifa wa Makao Makuu, alisema anaamini Mkutano Mkuu wa Copenhagen juu ya Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa ulikuwa ni wa mafanikio, kwa sababu kulipatikana maendeleo kwenye masuala kadha yanayohusu mada halisi ya mkutano, ikijumlisha ahadi za nchi wanachama kushirikiana kudhibiti bora halijoto kwenye maeneo yao isizidi kipimo cha daraja 2 za sentigredi (Celsius). Vile vile alisema Maafikiano ya Copenhagen yalijumlisha ahadi za nchi zenye maendeleo ya viwanda na nchi zenye maendeleo haba katika kupunguza kipamoja gesi chafu zinazomwagwa kwenye anga, katika awamu ya kati, na pia kukubaliana kuchangisha msaada wa fedha za kufadhiliwa nchi dhaifu ili kuziwezesha kukabiliana vizuri zaidi na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Aliongeza kusema Maafikiano ya Copenhagen huungwa mkono kifedha na mahitaji yake yana uwezo wa kutekelezwa. Kwa hivyo, alizihimiza nchi zote wanachama kuhakikisha Mfuko wa Copenhagen wa Kudhibiti Hali ya Hewa Kijani utachangishwa haraka iwezekanavyo. Vile vile KM alizisihi serikali zote kuunga mkono rasmi Maafikiano ya Copenhagen kwa kusajili na Taasisi ya UM juu ya Mfumo wa Kudhibiti Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC); na alisisitiza kwamba  nchi nyingi zikiridhia kutia sahihi mapatano, zitasaidia kurahisisha kufikia mapema mkataba utakaohishimiwa na wote.

Asubuhi, Baraza la Usalama lilifanyisha kikao cha hadhara, kuzingatia ripoti juu ya Sudan, ripoti iliowakilishwa kwenye ukumbi wa Baraza na mwakilishi wa Tume ya Hadhi ya Juu ya Umoja wa Afrika. Risala aliotoa KM kwenye mkutano ilieleza ripoti ya tume iliwapatia UM tathimini yenye uwazi, na imewasilisha fafanuzi hakika juu ya hali halisi Sudan, na ilipendekeza hatua kadha za kuchukuliwa kusukuma mbele amani. Ama kuhusu Darfur, KM alisema mpango wa amani wa eneo hili la Sudan magharibi sasa hivi umefikia hatua muhimu kabisa. Kwa hivyo, alitoa ombi kwa wajumbe wa Baraza la Usalama kuunga mkono, kwa msimamo ulio wazi, kazi za Mpatanishi Mkuu wa Darfur, Djibril Bassolé, utakaothibitisha ishara maalumu kwa makundi husika yote kwamba wakati umewadia kwa wao kujishirikisha zaidi na majadiliano ya upatanishi ili kurudisha utulivu na amani kwenye eneo lao. KM aliipongeza Tume ya Umoja wa Afrika kwa juhudi za kutayarisha mapendekezo yenye mawazo bunifu na yakinifu ya kutumiwa kushughulikia masuala magumu ya haki na upatanishi katika Sudan. Lakini pia KM alitilia mkazo kwamba ni lazima kwa Sudan kutekeleza azimio la Baraza la Usalama nambari 1591, linalohusikana na suala la Darfur, kwa uwiano wa mapendekezo ya Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki.