Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR imetangaza watu 74,000 wa Pembe ya Afrika wamehajiri Yemen 2009 kuomba hifadhi

UNHCR imetangaza watu 74,000 wa Pembe ya Afrika wamehajiri Yemen 2009 kuomba hifadhi

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti raia 74,000 waliwasili kwenye mwambao wa taifa la Yemen mwaka huu, kutoka eneo la Pembe ya Afrika, watu waliokuwa wakikimbia hali ya mtafaruku uliozuka na kujiepusha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, pamoja na uegugeu wa kisiasa, hali duni ya maisha, ikichanganyika vile vile na baa la njaa na ukame.

Idadi hii huwakilisha ongezeko la asilimia 50 la watu wanaohaajiri kutoka eneo hilo kutafuta hifadhi nchini Yemen. Mnamo 2008 shirika la UNHCR lilisajili raia 50,000 wa Pembe ya Afrika waliomba hifadhi Yemen. Miongoni mwa matatizo wanayokabiliwa wahamiaji hawa pale wanapojaribu kuvuka Ghuba ya Aden kutafuta hifadhi ni kwamba mara nyingi wahamiaji hupigwa na wavusha magendo, au hunajisiwa kimabavu, huuliwa na mara nyengine hutupwa baharini kwenye maeneo yaliofurika mapapa. Kadhalika, UNHCR inasema mashua nyingi zienye kubeba wahamiaji wa kutoka Pembe ya Afrika huwa zinajaa watu pomoni, hupinduka na kusababisha abiria kadha kuzama. Takwimu za UNHCR zimeonyesha wahamiaji 309 walizama na kufariki katika mwaka huu baada ya kujaribu kuvuka Ghuba ya Aden kwenye mashua zilizotumiwa na wafanya magendo.