Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UM yajihusisha Kenya kudhibiti mripuko wa kipindupindu Turkana Mashariki

Mashirika ya UM yajihusisha Kenya kudhibiti mripuko wa kipindupindu Turkana Mashariki

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti Alkhamisi jioni kwamba taasisi kadha za UM zinazohudumia misaada ya kiutu, hivi sasa zinajitahidi kuipatia Serikali ya Kenya misaada ya dharura inayohitajika kupambana na mripuko wa maradhi ya kipindupindu, yaliozuka kwenye eneo la kaskazini-magharibi, ambapo tumearifiwa watu karibu 30 walifariki kutokana na ugonjwa huo, kwenye zile sehemu za mbali zenye matatizo kuzifikia.

Ripoti zinaeleza watu zaidi ya 200 walishaambukizwa na kipindupindu kwenye eneo. Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limeanza kugawa vifaa vya afya, na zana za matunzo ya usafi vitakavyotumiwa hasa kwenye wilaya ya Turkana Mashariki, kwa lengo la kudhibiti maradhi yasienee zaidi kwenye eneo hilo. Kadhalika, OCHA imeripoti inashirikiana na Taasisi ya Taifa juu ya Operesheni za Kudhibiti Maafa pamoja na Wizara ya Afya ya Jamii nchini Kenya, kutathminia hali kwenye maeneo mawili ya nchi, yalioathiriwa na mripuko wa kipindupindu. Kwa mujibu wa OCHA, sibiko la vyanzo vya maji katika eneo la kaskakzini-magharibi ndio liliochochea mfumko wa maradhi ya kipindupindu kwenye eneo, kwa sababu ya kuselelea kwa ukame wa muda mrefu, hali iliowalazimisha wanavijiji na wakulima kutegemea maji ya visima, yanayotumiwa bia na wanyama wa mifugo pamoja na wanyama mwitu.