Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa Dunia wamo mbioni kuleta maafikiano ya kuridhisha kutoka Mkutano wa COP15

Viongozi wa Dunia wamo mbioni kuleta maafikiano ya kuridhisha kutoka Mkutano wa COP15

Majadiliano ya Mkutano Mkuu wa UM wa kuleta mapatano yatakayosaidia Mataifa Wanachama kudhibiti bora, kipamoja, athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika ulimwengu, Ijumaa yalishindwa kuwasilisha maafikiano ya kuridhisha, yaliotarajiwa kutiwa sahihi na viongozi wa Kitaifa na serikali 120 ziada waliokusanyika sasa hivi kwenye mji wa Copenhagen, Denmark.

Kwa mujibu wa ripoti za mwandishi habari wetu aliopo Copenhagen, Don Bobb, mabishano makali yalijadiliwa kwenye vikao vya faragha vilivyofanyika, takriban usiku mzima wa Alkhamisi ya jana, baina ya wawakilishi wa nchi tajiri na mataifa yanayoendelea. Viongozi wa dunia walijitahidi hadi asubuhi kuafikiana juu ya lugha ya azimio la kisiasa, la kuwakilishwa katika mwisho wa mkutano, azimio liliokuwa na mtazamo wa siku za baadaye, juu ya viwango vya kupunguza utoaji wa gesi chafu kwenye anga, vya kutekelezwa na mataifa yenye maendeleo ya viwanda, pamoja na kuzingatia mchango maridhawa wa kuyasaidia mataifa yanayoendelea kujirekibisha kimaendeleo, ili yaweze kukuza uchumi wao kwa taratibu zitakazotunza na kuhifadhi bora mazingira. Dalili ziliopo, kwa sasa hivi, zinaonyesha kuwepo utata mkubwa kwenye bidii ya kuleta mapatano yenye kufunga kisheria, maafikiano yatakayoidhinishwa na jamii nzima ya kimataifa. Hata hivyo, upenu uliojiri kwa sasa, unaashiria matumaini katika kupatikana maafikiano fulani kwenye majadiliano ya Copenhagen yatakayokuwa na natija "kwa ustawi wa umma wote wa kimataifa." Kuna tetesi majadiliano ya Mkutano wa Copenhagen, yaliotazamiwa kumalizika Ijumaa ya leo, huenda yakaendelea mpaka Ijumapili, tarehe 20 Disemba.