Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Alkhamisi asubuhi, mataifa 11 yaliripotiwa kuidhinisha na kuridhia Mapatano ya Kimataifa ya 2006 juu ya Mbao za Tropiki (2006 International Tropical Timber Agreement). Nyaraka za Mapatano ziliokusudiwa kukabidhiwa KM, ziliwakilishwa kwenye tafrija iliofanyika katika Ofisi ya UM juu ya Masuala ya Sheria. Mataifa 11 yalioridhia Mapatano ya Mbao za Tropiki ni kama ifuatavyo: Bulgaria; Jamhuri ya Ucheki; Finland; Ujerumani, Ireland; Ureno; Romania; Slovakia; Slovenia na Uspeni. Mapatano ya Mbao za Tropiki, bado hayajakuwa chombo rasmi cha kimataifa na sasa hivi kinajumlisha Makundi Yalioridhia mapatano kutoka nchi arobaini na moja.

Robert Serry, Mratibu Maalumu wa UM kwa Mpango wa Amani Mashariki ya Kati alipohutubia Baraza la Usalama mnamo siku ya leo, kuelezea hali katika eneo husika, alikumbusha ya kwamba katika kipindi ambapo mwaka 2009 unakaribia kumalizika, msururu wa matatizo umesalia, matatizo yenye kukwamisha na kuchelwesha suluhu ya amani katika Mashariki ya Kati. Alikumbusha mazungumzo ya amani baina ya Israel na Falastina yanaendelea kuzorota na yameshindwa kuanz, imani kati ya makundi yanayohusika na mzozo wa Mashariki ya Kati imeteremkia kiwango cha chini kabisa, "ukweli" wa kubuniwa unaendelea kuzushwa na kuenezwa kwenye ardhi zilizokaliwa kimabavu, na hali ya wasiwasi imeshtadi vilivyo kwenye mji wa Jerusalem. Aliongeza kusema vitendo vya Hamas na Israel havisaidii kuchangisha masilahi wala utulivu kwa umma unaoishi kwenye Tarafa ya Ghaza. Serry alionya pengo la kisiasa hatari huenda likazuka kwenye eneo; na pindi jumuiya ya kimataifa itashindwa kuleta mapatano ya mwisho, alitilia mkazo, hali ya amani itatuponyoka na itarudia vurugu la siku za nyuma na kuhatarisha utawala wa WaFalastina wenye mamlaka, na vile vile kutunyima ile suluhu ya kuwa na Mataifa-mawili. Alisema KM anatumai wapatanishi wa pande nne juuya Mashariki ya Kati watatekeleza, kidharura, majukumu yao, kwa kujumlisha ajenda ya pamoja mnamo miezi michache ijayo.