Operesheni za kijeshi Kongo Mashariki zitakamilishwa mwisho wa mwezi, asema Baraza la Usalama limearifiwa na Mjumbe wa UM katika JKK

17 Disemba 2009

Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa JKK, asubuhi aliwaeleza wajumbe wa Baraza la Usalama ya kuwa vikosi vya Serikali ya Kongo vimefanikiwa kuteka tena mji wa Dongo, katika jimbo la Equateur.

Wakati huo huo, operesheni za kijeshi zenye jina la Operesheni Kimia ya Pili, zinazoendelezwa Kongo mashariki, zinatarajiwa kukamilishwa mwisho wa mwezi huu, licha ya kuwa kadhia hiyo ilikabiliwa na matatizo kadha ya kiutu. Alihadharisha kwamba kundi la waasi wa Rwanda, la FDLR, lilioselelea kwa muda wa miaka kumi zaidi, bado linaendelea kuhatarisha usalama na amani kwenye majimbo ya Kivu. Alisema chini ya amri ilioidhinishwa leo hii na Serikali ya JKK, vikosi vya Ulinzi Amani vya UM (MONUC) pamoja na Vikosi ya Jeshi la JKK vitalenga juhudi zao katika kushikilia yale maeneo yaliokombolewa karibuni kutoka waasi wa FDLR na kujitahidi kuwakinga raia mashambulio kwenye maeneo yaliokosa ulinzi unaofaa. Doss alisema kumezuka vizingiti kadha vyenginevyo vinavyoendelea kutatanisha operesheni za amani katika JKK, hasa katika ulinzi wa raia, hifadhi ya watu waliong'olewa makazi na wahamiaji wa ndani ya nchi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter