Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

A. Guterres anakumbusha, mabadiliko ya hali ya hewa yanahusiana na watu kung'olewa mastakimu, mapigano na uhamaji

A. Guterres anakumbusha, mabadiliko ya hali ya hewa yanahusiana na watu kung'olewa mastakimu, mapigano na uhamaji

Vile vile tukizungumzia matukio kwenye Mkutano wa COP15 unaofanyika Copenhagen, Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Huduma za Wahamiaji, aliwaambia wajumbe wa kimataifa Ijumatano kwamba zipo fungamano halisi kati ya watu kuhamahama makwao, kung\'olewa makazi na taathira za mabadiliko ya hali ya hewa.

Alisisitiza kwamba katika kipindi cha hivi sasa, kuna ukungu kwenye tafsiri ya tofauti za kikawaida, baina ya wahamiaji wanaotafuta usalama na wahamaji, kwa sababu ya mchanganyiko wa vipengele kadha, vyenye kuchochea watu kuhajiri makwao - ikijumlisha madhara yanayoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa, ukosefu wa chakula, hali duni na ufukara, pamoja na mapigano yanayofumka mara kwa mara - kadhia ambazo, alitilia mkazo, huwalazimisha watu kuamua kutafuta hifadhi na ajira nje ya makwao. Alisema mabadiliko ya hali ya hewa, kwa sasa hivi, ndio yenye kuongoza uchocheaji wa watu kung'olewa makazi, kwa sababu mazingira kama haya mara nyingi huzusha mapigano, hasa pakiwepo mashindano kati ya makundi ya raia, kupata rasilmali adimu kwa sababu ya hali ya hewa isiofuata majira ya kimaumbile.