Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon Ijumatano alihudhuria tafrija maalumu mjini Copenhagen, Denmark kuanzisha mradi wa Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) wa kubuni "jiko la stovu salama" ambalo litatumiwa bila kuunguza kuni. Jiko hili litasaidia kutunza miti kwa kuhakikisha haitokatwa, na litapunguza tatizo la kumwaga gesi chafu kwenye anga kwa sababu ya kuchoma kuni, na vile vile kuyanusuru maisha ya wanawake na watoto wa kike, ambao mara nyingi hulazimika kwenda masafa marefu kukusanya kuni, shughuli ambazo husababisha wanawake kushambuliwa, kuibiwa mali zao na hata hunajisiwa kimabavu na wavunjaji sheria. Mradi wa WFP hasa umekusudiwa kuwasaidia wanawake wa Uganda na Sudan. Jiko la stovu salama jipya litatengenezwa mwaka ujao, na litagaiwa wahamiaji milioni 6, waliopo katika nchi 36, wakijumuisha vile vile watu waliong\'olewa makazi na wale raia wanaorejea makwao kutoka nchi za nje ambapo walipatiwa hifadhi na usalama.

Msemaji mpya wa KM, anayeitwa Martin Nesirky, katika kujibu suala kuhusu sababu zinazochelewesha waandishi habari kuhudhuria, kwa wakati, majadiliano ya Mkutano wa UM juu ya Mabadiliko ya Halihewa, yanayofanyika kwenye Jumba la Kituo cha Bella, kiliopo Copenhagen, alisema UM unasikitika juu ya ucheleweshaji wa muda mrefu wa wajumbe wanaotaka kuingia mkutanoni, hasa wale wanaowakilisha mashirika yasio ya kiserikali (NGOs) ambao vile vile hucheleweshwa pale wanapokwenda kuchukua vitambulisho rasmi vya mkutano. Msemaji wa KM alisisitiza UM unajitahidi, kwa kila njia, kuhakikisha matatizo haya yanasuluhishwa kidharura. Watu 45,000 ziada walisajiliwa kuomba kuhudhuria mkutano, na fungu kubwa la wale waliotuma ardhilhali zao waliwasili Copenhagen mwanzo wa wiki, Ijumatatu, na walisababisha msongomano mkubwa kwenye maeneo ya nje ya jumba la mkutano, mahali yaliopo chini ya ulinzi wa polisi wa Denmark. Ama kuhusu utaratibu wa kuruhusu idadi ya kikomo ya wawakilishi wa mashirika yasio ya kiserikali (NGOs) kuhudhuria mikutano, UM umeeleza mfumo huu utaendelea kutumiwa na watayarishaji mkutano. Wawakilishi wa NGOs wamepewa nusu ya nafasi ya ukumbi wa mkutano kwenye Kituo cha Jumba la Bella, fursa ambayo haijawahi kupatiwa jumuiya za kiraia katika vikao vya siku za nyuma vinavyohusu mazungumzo ya mabadiliko ya hali ya hewa.