Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwasili kwa KM Copenhagen kunatazamiwa kuhamasisha mataifa kukamilisha mapatano ya COP15

Kuwasili kwa KM Copenhagen kunatazamiwa kuhamasisha mataifa kukamilisha mapatano ya COP15

Ilivyokuwa majadiliano ya Mkutano Mkuu wa UM juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa yanaonekana kupwelewa, na yamezorota kwenye mabishano ya kiutaratibu, pamoja na mivutano na mgawanyo mkubwa wa kimasilahi baina ya nchi tajiri na mataifa maskini,

inaaminika kwamba kuwasili kwa KM Ban Ki-moon Ijumanne kwenye jiji la Copenhagen, kutasaidia kuhamasisha wajumbe wa kimataifa, wanaohudhuria vikao vya viwango vya mawaziri, kufikia mapema itifaki inayohitajika kusukuma mbele mapatano yao. Nchi nyingi zenye maendeleo ya viwanda zinatarajia mnamo mwisho wa Mkutano wa Copenhagen, ile Itifaki ya Kyoto itaunganishwa na matokeo ya Mkutano, na kuwakilisha mapatano ya mkataba mmoja tu. Lakini, hata hivyo, mataifa yanayoendelea, ambayo hayahusikani kamwe na uchafuzi wala utoaji wa gesi chafu kwenye anga, wanasisitiza Itifaki ya Kyoto iendelee kutumiwa kimataifa kuongoza udhibiti wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa, na wangelipendelea kuona Itifaki ya Kyoto itatumiwa kupita 2012, pale ambapo awamu ya kwanza ya mapatano haya itamalizika. Vile vile mataifa yanayoendelea yanataka kupatikane maafikiano ziada, pekee, kufuatia majadiliano ya Copenhagen yanayotazamiwa kumalizika mwisho wa wiki. Yvo de Boer, Mkurugenzi Mkuu wa Tassisi ya UM juu ya Mkataba wa Kudhibiti Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC) alihadharisha Mataifa Wanachama wakumbuke majadiliano ya Copenhagen hayajakusudiwa kutafsiriwa kama ni majaribio ya "kushindilia na kulazimisha masilahi ya walio wachache yaridhiwe kimabavu na walio wengi." Alisisitiza majadiliano ya Copenhagen yamekusudiwa hasa "kuwashirikisha walio wengi kwenye juhudi za kuzingatia masilahi ya umma wote wa kimataifa."