Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ofisi ya UM Juu ya Misaada ya Dharura (OCHA), imetangaza ripoti yenye kuelezea utaratibu wa sheria unaotumiwa na utawala wa kimabavu wa Israel katika kugawanya ardhi za WaFalastina ziliopo kwenye kanda mbalimbali za sehemu ya Ukingo wa Magharibi ya Mto Jordan, sehemu inayotambuliwa kama Eneo la C. Chini ya mfumo huo, WaFalastina huwa hawaruhusiwi kuendeleza ujenzi wa aina yoyote kwenye asilimia 70 ya maeneo yao. Wakati huo huo, ile asilimia 30 iliosalia ya maeneo ya WaFalastina, kumewekwa msururu wa vizuizi na vikwazo aina kwa aina ambavyo vinafuta, takriban, fursa zote za mtu kupata kibali cha kujenga. Kutokana na vikwazo kama hivi, makumi elfu ya WaFalastina wenye azma ya kujenga kwenye Eneo la C hunyimwa, kwa makusudi na kwa mipangilio, fursa ya kisheria ya kujenga na kutosheleza mahitaji ya makazi yao. Kwa sababu hizo,WaFalastina hulazimika kuendeleza ujenzi wa makazi yao bila ya kibali kutoka kwa watawala walowezi. Kwa hivyo, raia wa KiFalastina hukabiliwa na hatari ya majumba yao kubomolewa na, halafu, hung\'olewa makazi na watawala wa Israel waliokalia kimabavu ardhi yao.

Ijumatatu, kwenye mji wa Cairo, Shirika la UM Linalofarajia Wahamiaji wa KiFalastina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA) lilianzisha kampeni ya kuchangisha Msaada wa Dharura kwa 2010 wakati Mataifa Wanachama wa Umoja wa Nchi za Kiarabu yalipokutana nchini Misri. UNRWA ilipendekeza ifadhiliwe na nchi za Kiarabu msaada wa dola milioni 323, ambazo zitatumiwa kuhudumia miradi ya kuzalisha ajira, na katika kuimarisha huduma za ilmu, afya bora na ulinzi kwa WaFalastina. Kwenye tafrija ya kuanzisha kampeni hiyo, Kamishna Mkuu wa UNRWA, Karen AbuZayd, alieleza kwamba mnamo miezi 12 iliopita, ilibainika dhahiri, kukithiri kwa nguvu zaidi mizozo kwenye maeneo yaliokaliwa ya WaFalastina, kuanzia yale mashambulio na uvamizi wa majeshi ya Israel kwenye Tarafa ya Ghaza. Vikwazo vilioekewa Ghaza tangu kipindi hicho, ilieleza UNRWA, vilisababisha matokeo yalioangamiza vipengele vyote vya maisha kwa watu milioni 1.4 walionaswa kihali katika Ghaza.