Mkuu wa UNFCCC abainisha mapatano yamefikiwa kwenye teknolojiya kinga dhidi ya gesi chafu angani

12 Disemba 2009

Mkuu wa Taasisi ya UM juu ya Mkataba wa Kudhibiti Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC) kwenye mahojiano ya Alkhamisi na waandishi habari mjini Copenhagen, alisema wajumbe wa kimataifa, kwa sasa, wameshafikia makubaliano juu ya taratibu za kuanzisha mfumo mpya wa teknolojiya ilio imara na madhubuti,

itakayotumiwa kukabiliana na madhara yanayotokana na uchafuzi wa anga, unaosababishwa na vitendo vya wanadamu, pindi fedha maridhawa zitakusanywa kwa ukamilifu kutoka nchi wanachama. Utaratibu huu unapendekeza kuwepo Bodi la Utendaji litakalodhaminiwa madaraka ya kusimamia maendeleo ya kuharakisha ubunifu wa teknolojiya mpya ya marekibisho, ili kuyasaidia mataifa waathirika na mabadiliko ya hali ya hewa. De Boer alitarajia Raisi wa Mkutano Mkuu wa Copenhagen, yaani Mkutano wa COP ya 15, atatathminia maendeleo ya majadiliano mwisho wa wiki hii. Juu ya kuendelea kutumiwa kwa Mkataba wa Kyoto, de Boer alisema itifaki hii ni lazima idumishwe kwa sababu ndio chombo pekee cha kimataifa, chenye uzito wa kisheria, ilioridhiwa na fungu kubwa la Mataifa Wanachama dhidi ya taathira haribifu za mageuzi yanayotokana na hali ya hewa ya kigeugeu. Alisema vile vile kunahitajika muda wa kutosha kuruhusu nchi wanachama kuridhia na kuidhinisha maafikiano mapya kabla mapatano haya hayajafanywa kuwa sheria ya kimataifa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud