Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wawakilishi wa G-77 waamini kuna rasilmali za kutosha ulimwenguni kukomesha madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa

Wawakilishi wa G-77 waamini kuna rasilmali za kutosha ulimwenguni kukomesha madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa

Wawakilishi wa Mataifa wanachama wa Kundi la G-77 na Uchina, wamesisitiza kwenye kauli kadha walizowasilisha kwenye majadiliano ya Copenhagen ya kuwa umma wa kimataifa, kwa ujumla, katika karne ya ishirini na moja, umebarikiwa rasilmali ya kutosha kushughughulikia, kwa mafanikio, matatizo

yote yanayohusu udhibiti wa pamoja wa athari haribifu na chafuzi zinazoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa katika dunia, hasa katika ile kadhia ya kupunguza utoaji wa gesi chafu kwenye anga. Marekani ilipendekeza kima cha utoaji wa gesi chafu na haribifu kwenye anga kipunguzwe kwa asilimia 4. Lakini kwenye mazungumzo na waandishi habari mjini Copenhagen Alkhamisi ya leo, Lumumba Stanislaus Di-Aping wa Sudan, Mwenyekiti wa Kundi la G-77 na Uchina, linalowakilisha nchi zinazoendelea 132, alisisitiza pendekezo la Marekani halimudu kamwe jukumu la kuhifadhi ulimwengu na athari haribifu za mabadiliko ya hali ya hewa. Aliiomba Marekani izingatie tena, athari za muafaka uliokubaliwa na wanachama wa Kundi la G-8, wanaowakilisha nchi zenye maendeleo ya viwanda, ambao ulipendekeza kuwekwa kiwango cha daraja 2 za sentigredi kwenye bidii za kudhibiti hali ya hewa ya mazingira yetu, licha ya kuwa kima hiki, kwa mujibu wa taarifa za wanasayansi wa kimataifa, kikiendelezwa kinaashiriwa kitahatarisha maisha, katika bara zima la Afrika kwa ujumla, na kuzusha mateso kwa umma yaliopita kiasi. Alikumbusha, "ulimwengu umejaaliwa rasilmali za kutosha kusuluhisha, kwa nguvu zaidi, na kidharura, matatizo yanayoambatana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa yaliojiri kwa sasa hivi katika dunia."