Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP kutumia msaada Umoja wa Ulaya kufyeka utapiamlo mkali unaofukuta Kenya Kaskazini

WFP kutumia msaada Umoja wa Ulaya kufyeka utapiamlo mkali unaofukuta Kenya Kaskazini

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kwamba yuro milioni 7.5 (sawa na dola milioni 11.3) ilizopokea kutoka Idara ya Misaada ya Kiutu ya Kamisheni ya Mataifa ya Ulaya, zitatumiwa kuhudumia kihali matatizo ya utapiamlo wa kima cha juu, yaliojiri miongoni mwa watoto wadogo, mama wajawazito na mama wanaonyonyesha wanaoishi katika maeneo ya ukame, Kenya Kaskazini.

Uchunguzi juu ya lishe ulioendelezwa karibuni kwenye eneo hilo, umeonyesha kuwepo utapiamlo mkuu miongoni mwa wakazi wa wilaya za Kenya Kaskazini - kima kilichokiuka asilimia 15 ya kigezo cha dharura. Ikiwa miongoni mwa juhudi za kupunguza njaa kwenye eneo hilo, kuanzia mwezi Disemba, WFP inaendeleza operesheni za miezi minne zilizokusudiwa kuwapatia chakula watoto chini ya umri wa miaka mitano kwenye wilaya husika, pamoja na kufadhilia chakula kwa mama wajawazito na mama wanaonyonyesha, na vile vile kuwafadhilia mchanganyiko wa chakula ziada, kilichorutubishwa mahindi na maharagwe ya soya pamoja na mafuta ya mbogamboga. Hatua hii ilichukuliwa kwa sababu ya matatizo ya ukame mkali uliotanda Kenya Kasklazini, katika miezi ya karibuni, na kutokana na bei ya juu ya chakula.