Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa wafunguliwa rasmi Copenhagen

Mkutano wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa wafunguliwa rasmi Copenhagen

Mkutano Mkuu wa UM juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa, unaojulikana kama Mkutano wa COP 15, umefunguliwa rasmi Ijumatatu ya leo, kwenye mji wa Copenhagen, Denmark ambapo viongozi wa kimataifa walinasihiwa na Mkuu wa Mkutano, Yvo de Boer, kwamba, baada ya muda mrefu wa mivutano na majadiliano ya huko na kule, wakati umewadia kwa walimwengu kuchukua vitendo halisi dhidi ya athari haribifu zinazochochewa na mabadiliko ya hali ya hewa katika dunia.

Ujumbe huu ulinasihiwa wawakilishi 200 wa Mataifa Wanachama, wanaohudhuria mkutano wa Copenhagen. Yvo de Boer, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya UM kuhusu Mkataba wa Kudhibiti Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC) alisema "ratiba ya saa ya kamsa imeshagonga sufuri [na] baada ya miaka miwili ya mahojiano, wakati umeshawadia kutimiza ahadi [ya miradi ya kupambana na athari haribifu zinazoangamiza utulivu maumbile wa hali ya hewa]). Mwenyekiti wa Mkutano wa Copenhagen, Connie Hedegaard wa kutoka Denmark alihadharisha kwenye risala aliotoa kwenye ufunguzi wa kikao ya kuwa "hakuna anayeweza kupinga ushahidi uliothibitishwa na matukio ya kisayansi kuhusu kujiri kwa athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani .. katika mazingira ambayo suluhu maridhawa zipo za kulitatua suala hili .. pamoja na imani ya kisiasa imara kabisa." Alisisitiza wakati wa vitendo ni hivi sasa. Kwa mujibu wa taarifa za UM, viongozi 100 ziada wa kiserikali na kitaifa, wanatarajiwa kuhudhuria hatua ya mwisho ya Mkutano wa Copenhagen utakaochukua siku kumi na mbili.