Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Matokeo ya uchunguzi ulioendelezwa na Nicholas Stern, Mwenyekiti wa Taasisi ya Utafiti ya Grantham juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa, iliopo kwenye Chuo Kikuu cha London School of Economics (LSE), akijumuika na Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) yameonyesha dhahiri kuwepo uwezekano wa kutia moyo, kwa nchi zilizokusanyika Copenhagen, Denmark kuhudhuria Mkutano Mkuu wa UM juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa, kufikia itifaki ya kupunguza utoaji wa gesi chafu angani. Hatua hii itausaidia ulimwengu kuepukana na madhara ya kuongezeka kwa halijoto, kwa kiwango cha daraja 2 ya sentigredi. Fafanuzi za ripoti ya utafiti ziliochapishwa kwenye mkesha wa Mkutano wa UM juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa, zimethibitisha kuwepo pengo la tani bilioni chache tu kuhusu kiwango kinachotakikana kupunguzwa kila mwaka, kitaifa, cha zile gesi chafuzi zinazomwagwa angani. Imetangazwa na Ofisi ya Msemaji wa Ban Ki-moon hii leo kwamba KM atawasili Copenhagen wiki ijayo kuhudhuria kikao cha hadhi ya juu cha Mkutano Mkuu wa UM juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa, kikao ambacho kinatarajiwa kuanza Ijumanne alasiri, katika tarehe 15 Disemba 2009. KM anaamini Mkutano Mkuu wa Copenhagen utawasilisha kipindi muhimu cha mabadiliko kwenye bidii za kimataifa za kudhibiti athari za hewa chafuzi kabla mageuzi haya kutuponyoka, tukishindwa kuwakilisha enzi mpya ya "ukuaji wa kijani" wa uchumi na jamii wenye natija za kimaisha kwa wote.

Ad Melkert, Mjumbe Maalumu wa KM (MMKM) kwa Iraq, amewapongeza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kukamilisha Sheria ya Uchaguzi, iliojumlisha kila mtu na kutoka matabaka yote ya kijamii. Melkert alisema mnamo wiki chache zilizopita, Shirika la UM la Usaidizi Amani katika Iraq (UNAMI), lilishirkiana kwa makini na bidii kuu na wajumbe wa Baraza linalowakilisha vyama na makundi yote ya kisiasa, kurahisisha kubuni mfumo uliosaidia kufikiwa kwa mapatano yalioridhisha wahusika wote. Alisema UNAMI ilishauri makundi yote juu ya uwezekano wa kuitisha uchaguzi kwenye Ijamamosi ya tarehe 27 Februari 2010. UM umesisitiza kuwa upo tayari kuhakikisha kamisheni ya uchaguzi ya Iraq itapatiwa kila msaada unaohitajia kutekeleza kadhia hiyo.

Ijumapili KM alizungumza na Raisi Omar Hassan al-Bashir wa Sudan kujadilia tatizo la dharura la kiutu pekee, ambapo aliombwa kutumia wadhifa wake kusaidia kuachiwa watumishi wawili wa Shirika la Mchanganyiko la UM-UA kwa Darfur (UNAMID) ambao walitekwa nyara tangu 29 Agosti (2009) na wameshikwa hivi sasa kwa zaidi ya siku 100. Serikali ya Sudan imeripotiwa kujaribu kusaidia kuachiwa kwa watumishi wa UNAMID lakini bado hawajafanikiwa. Inasemekena hali ya mmoja wa mateka hawa ni mbaya sana na ni ya hatari. Kadhalika, KM ameomba waliofanya makosa ya kuhujumu walinzi amani wa UNAMID, mnamo mwisho wa wiki mbili zilizopita katika Darfur Kaskazini, ambapo wanajeshi watano wa Rwanda waliuawa, wakamatwe na wafikishwe mahkamani kufanyiwa kesi. Raisi al-Bashir alieleza kwamba ametoa ilani maalumu inayoyataka mashirika ya usalama ya kizalendo yajitahidi kuwasaka na kuwatia mbaroni, haraka iwezekanavyo, wakosaji wa matukio hayo. Katika kumaliza mazungumzo yao ya simu KM Ban Ki-moon alitoa shukrani zake kwa msaada wa Serikali ya Sudan juu ya uteuzi wa Ibrahim Gambari kuwa Mjumbe Maalumu wa Pamoja wa UNAMID.

Vile vile kuhusu Sudan, Ashraf Jehangir Qazi, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Sudan ameeleza kuingiwa wasiwasi kwa kuwekwa kizuizini na kupigwa kwa viongozi mashuhuri wa kundi liliokuwa la waasi la SPLM, pamoja na wafuasi wa vyama vya upinzani na wanaharakati wa jumuiya za kiraia, pale walipoandamana kwenye mdhahara uliofanyika mapema Ijumatatu. Kadhalika, KM alisema ana wahka na ripoti kuhusu kutiwa moto ofisi za Chama kinachotawala Sudan cha NCP. Matukio haya yanakhofiwa huenda yakazusha taathira mbaya dhidi ya utekelezaji wa yale Mapatano ya Jumla ya Amani (CPA) katika Sudan katika kipindi muhimu cha majadiliano ya kuimarisha utulivu baina ya NCP na SPLM.