Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM inahimiza kujumuishwa kwenye miradi ya MDGs mahitaji ya walemavu na walionyimwa uwezo

UM inahimiza kujumuishwa kwenye miradi ya MDGs mahitaji ya walemavu na walionyimwa uwezo

Kama mlivyosikia kwenye taarifa za habari wiki hii, kwamba Alkhamisi ya tarehe 03 Disemba (2009) iliadhimishwa hapa Makao Makuu ya UM, kuwa ni Siku ya Kimataifa kwa Watu Walemavu na Wenye Kunyimwa Uwezo wa Kimaumbile.

Mada ya taadhima za 2009 ilitilia mkazo zaidi umuhimu na ulazima wa kuambatanisha masuala yanayohusu haki za walemavu na walionyimwa uwezo wa kimaumbile, kwenye ile miradi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs), ili kupunguza hali duni na ufukara duniani itakapofika 2015. Mtayarishaji vipindi, wa idara ya Kiingereza ya Idhaa ya Redio ya UM, Dianne Penn, alichukua fursa ya taadhima hizo kuzungumza na mkuu wa Kitengo cha UM juu ya Haki za Watu Walemavu, anayeitwa Akiko Ito. Bi Ito alifungua mahojiano yao kwa kuelezea umuhimu wa kujumuisha masuala ya walemavu kwenye miradi ya MDGs:

CUT:   "Bila ya kutamkwa kidhahiri, tunaweza kusema watu walemavu

huwakilisha sehemu moja ya vipengele vya sera za kutekeleza ile miradi ya MDGs ulimwenguni. Lakini, kwa wakati huo huo tutaona walemavu hawaonekani kwenye shughuli za kutekeleza malengo ya MDGs. Kwa mfano, walemavu hawakutajwa, abadan, kwenye orodha ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia; na suala la ulemavu, wenyewe, nalo pia halikujumlishwa kwenye viashirio vinavyopima huduma za MDGs, na kuna takwimu chache sana ulimwenguni zenye kubainisha mafanikio halisi ya walemavu au yale mafanikio ya watu walionyimwa uwezo wa kimaumbile, kwenye mchango wao wa kuyafikia Malengo ya Milenia."

AZR:    Bi Ito alijaribu kutupatia mifano michache ambayo ilithibitisha madai yake ya kuwa walemavu hunyimwa haki za kujiendeleza kiuchumi na kijamii, kwa uwiano na mapendekezo ya MDGs ya kupunguza ufukara na njaa na elimu ya msingi kwa wote:

CUT:    "Naweza kusema, mfano mzuri, ni ule unaowahusu walemavu wanawake. Kuna miradi mingi ulimwenguni, yenye kutoa huduma za afya ya uzazi, lakini hakuna huduma maalumu ya afya ya uzazi iliowalenga wanawake walio walemavu pekee. Mathalan, tutaona wanawake walemavu wanaopata mimba, mara nyingi hukoseshwa matunzo yanayoridhisha, na baadhi ya wakati hukosa hata uwezo wa kufikia vituo vya afya vyenye uangalizi unaofaa, na hupambwa na matatizo kadha mengineyo kama hayo. Kwa hivyo, ikiwa wanawake walemavu wataweza kupata huduma za afya, zenye kutosheleza, kama watu wa kawaiada, bila ya shaka watoto watakaozaliwa nao watakuwa na siha njema, hali ambayo itamaanisha nasi vile vile tutakuwa tunachangisha, kwa utaratibu unaofaa, katika kutekeleza lile lengo la MDGs, la kuendeleza huduma bora za uzazi."

AZR: Kwenye sherehe za mwaka huu, kuadhimisha Siku ya Kimataifa kwa Watu Walemavu na Wenye Kunyimwa Uwezo wa Kimaumbile, zilizofanyika hapa Makao Makuu, alihudhuria vile vile msanii maarufu Mmarekani, mwenye asili ya KiAfrika, anayeitwa Stevie Wonder, ambaye aliteuliwa rasmi na KM kuwa Mjumbe wa Amani wa UM. Stevie Wonder ni mwimbaji aliokosa uwezo wa kuona, maana yeye ni kipofu tangu alipozaliwa. Tulitaka kujua kuwepo kwake kwenye taadhima za mwaka huu za UM kulimaanisha nini, hasa kwa wenzetu walio walemavu? Kwa mara nyengine tena Akiko Ito, wa kutoka Kitengo cha UM juu ya Haki za Watu Walemavu:

CUT:    "Kwa kweli, ilikuwa ni ndoto kwa kitengo chetu, kwa sababu tulishauriana, kwa muda mrefu, karibu miaka 10, juu ya hii rai ya kumwalika Stevie Wonder kuja Makao Makuu, kuhudhuria Siku ya Kimataifa, kama ninavyokumbuka! Kwa sababu huyu ni msanii mmoja mwenye kujumlisha maadili yetu yote; anawakilisha ujumbe halisi wa taasisi yetu. Kwa sababu tukimkumbuka Stevie Wonder, huwa tunakumbuka umahiri na uwezo alionao, tunafikiria kipaji kikubwa na kipawa alicho nacho cha kisanii, tunazingatia mchango wa usanii alionao wa kiwango cha juu kabisa, ambao siku zote yeye yupo tayari kugawana na kila mtu ulimwenguni. Kwa hivyo, sifikiri ni ulemavu unaomzuia mtu kutenda makuu, bali ukosefu wa uwezo, labda, na maajaliwa ya kipaji. Na huu ndio ujumbe ambao UM unajaribu kuuwasilisha ulimwenguni: yaani kama maisha ya Stevie Wonder yanavyoonyehsa, ulemavu alionao wa kupoteza nuru ya macho ni maumbile, lakini haukumzuia kutenda makuu maishani mwake pale alipojaaliwa uwezo, kilicho muhimu kukumbuka ni vipaji vyetu vya kibinafsi pekee sio vinavyotupatia maendeleo na kutusaidia kufikia malengo yetu bila ya uwezo."

Hiyo likuwa ni tafsiri ya kauli ya Akiko Ito, mkuu wa Kitengo cha UM juu ya Haki za Watu Walemavu, akizungumzia juu ya sera ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa kwa Watu Walemavu na kwa Wenye Kunyimwa Uwezo wa Kimaumbile. Na tutamaliza yetu kwa muziki wa Stevie Wonder.