Mkutano wa Cartagena umepitisha azimio la kukomesha mateso ya silaha zilizotegwa
Kwenye Mkutano Mkuu wa Mapitio juu ya Ulimwengu Huru dhidi ya Silaha za Mabomu Yaliotegwa Ardhini, unaofanyika kwenye mji wa Cartagena, Colombia, Mataifa Wanachama yalioidhinisha na kuridhia Mkataba wa Kupiga Marufuku Mabomu Yaliotegwa, yameahidi tena kukomesha usumbufu na madhara yanayoletwa na silaha hizo.
Mataifa yalipitisha azimio la mpango wa utendaji, wa miaka mitano, utakaoyaongoza mataifa husika kusafisha maeneo yalioambukizwa na mabomu yaliotegwa ardhini, na kuwasaidia kihali waathirika wa silaha hizo, na vile vile kuhakikisha akiba iliosalia ya vijibomu viliotegwa itaangamizwa milele. Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), kwa kuhusiana na Mkutano wa Cartagena, limetangaza taarifa yenye kuipongeza Rwanda, baada ya taifa hilo kutangazwa Alkhamisi, kuwa ndio taifa la mwanzo ulimwenguni kufanikiwa kufyeka mabomu yaliotegwa kwenye ardhi. Katika miaka ya mwisho ya 1990, Wizara ya Ulinzi ya Rwanda ilichukua hatua maalumu ya kuanzisha operesheni za jumla za kuondosha na kusafisha zile silaha ziliotegwa chini ya ardhi kwenye eneo lao, mradi ambao ulisaidiwa na serikali kadha za kimataifa, pamoja na mashirika yanayohusika na huduma za maendeleo, ikijumlisha UNICEF.