Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio la Mogadishu ni pigo adhimu kwa maendeleo ya afya Usomali, imeonya WHO

Shambulio la Mogadishu ni pigo adhimu kwa maendeleo ya afya Usomali, imeonya WHO

Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kupitia msemaji wake wa Geneva, Fadela Chaib, limeripoti leo Ijumaa ya kuwa shambulio la Alkhamisi la bomu la kujitoa mhanga, liliotukia Mogadishu, ni pigo lenye msiba mkubwa katika sekta ya afya ya Usomali.

Miongoni mwa watu 15 waliouawa na shambulio hili alikuwemo Waziri wa Afya wa Usomali, Dktr. Qamr Aden Ali, pamoja na baadhi ya wakuu wa serikali na jamii. Tukio hili, ilisema WHO, linabainisha dhahiri kwamba kuna haja kubwa ya kurudisha haraka hali ya utulivu na usalama katika nchi. Kwa mujibu wa WHO, Dktr. Ali alikuwa mtetezi wa afya asiyechoka kazi, na alionyesha uwezo na bidii kubwa katika kuendeleza viwango vya afya na matunzo bora ya afya kwa umma wa Usomali, kwa ujumla. Dktr. Ali alishirikiana kwa ukaribu zaidi na shughuli za WHO katika maamirisho ya mfumo wa afya nchini Usomali. Shambulio lilitukia wakati wa taadhima za kutoa shahada kwa wanafunzi waliohituimu masomo ya udaktari kwenye Chuo Kikuu cha Banadir, taasisi ya mafunzo ya udaktari inayofundisha Wasomali watakaosaidia kuhudumia afya mamilioni ya raia wenziwao, ambao wanaendelea kuteseka na mzozo wa kiutu ulioselelea nchini kwa miongo kadha.