Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wahimiza kuwapatia mamlaka ya kujitegemea watu wenye ulemavu

UM wahimiza kuwapatia mamlaka ya kujitegemea watu wenye ulemavu

UM leo unaadhimisha rasmi Siku ya Kimataifa kwa Watu Walemavu na Wenye Upungufu wa Uwezo.

Kwenye risala ya KM kuadhimisha na kuihishimu siku hii, aliyasihi Mataifa Wanachama kutosahau kuwafikiria watu milioni 800 walemavu na walionyimwa uwezo waliopo ulimwenguni, pale wanapozingatia juhudi za kufikia malengo ya maendeleo juu ya ustawishaji wa viwango vya kihali na maisha bora kwa kila mtu. Alikumbusha, watu walemavu hukabiliwa na matatizo ya kila aina, na wengi wao hukutikana kwenye jamii za watu maskini na mara nyingi huwa wanatengwa kijamii. Licha ya kuwa watu walemavu wamekabiliwa na vizingiti vigumu kwenye maisha yao, hata hivyo bado "wanaendelea kuonyesha bidii ya kujiendeleza kimaisha na wamefanikiwa kufikia maendeleo makubwa, aina kwa aina, katika ngazi zote za maisha ya wanadamu," alisema KM. Mada ya mwaka huu kuhusu Siku ya Kimataifa kwa Watu Walemavu na Wenye Upungufu wa Uwezo imetilia mkazo umuhimu wa "kujumlisha masuala ya ulemavu kwenye Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs)." Vile vile katika siku ya leo, msanii maarufu wa KiMarekani, Stevie Wonder, ambaye pia ni mwimbaji mashuhuri wa dunia na mtunzi wa nyimbo zinazotambuliwa katika sehemu nyingi za ulimwengu, alihudhuria baadhi ya taadhima za Makao Makuu zilizofanyika hii leo kuhusu Siku ya Kimataifa kwa Walemavu na Wenye Upungufu wa Uwezo. Kadhalika, KM leo alimteua rasmi Stevie Wonder kuwa ni Mjumbe wa Amani kwa UM na anatarajiwa kutetea haki za watu wenye ulemavu ulimwenguni, hasa ilivyokuwa yeye mwenyewe binafsi alipoteza nuru ya macho tangu alipozaliwa.