Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ripoti mpya ya KM kuhusu shughuli za Ofisi ya UM ya Huduma za Mchanganyisho za Amani Burundi (BINUB) imewakilishwa Alkhamisi ya leo hapa Makao Makuu. Ndani ya ripoti KM alibainisha kwamba tangu BINUB kuanzishwa nchini kulishuhudiwa maendeleo mengi, ya kutia moyo. Lakini ilisema ripoti hali bado ni ya wasiwasi na dhaifu. Kwa mujibu wa ripoti, mwaka ujao utakuwa muhimu kwa Burundi, na taifa litahitajia kusaidiwa na jamii ya kimataifa ili kuhakikisha maendeleo yaliofikiwa hadi sasa kuwa yataimarishwa vizuri zaidi kabla, na baada, ya uchaguzi wa 2010, na wakati wa upigaji kura, hali kadhalika. Kwa hivyo, KM amependekeza shughuli za Ofisi ya BINUB ziendelee kutekelezwa Burundi kwa mwaka mmoja zaidi, baada ya muda uliodhaminiwa na Baraza la Usalama kwa sasa kumalizika mnamo tarehe 31 Disemba 2009.

Alkhamisi asubuhi, KM alimjulisha rasmi, mbele ya wajumbe wa kimataifa waliokusanyika Makao Makuu, yule msanii mashuhuri wa KiMarekani, Stevie Wonder kuwa ni Mjumbe wa Amani mpya kwa UM. Alikiri KM kwenye risala yake kwamba Stevie Wonder ni mutribu maarufu, na ni msanii mkubwa anayetambulikana takriban kote ulimwenguni. Lakini vile vile, KM alikumbusha, msanii huyu ni mwanaharakati shupavu na mfadhili mkubwa wa misaada ya kiutu kwa fungu kubwa la umma wa kimataifa ulionyimwa fursa ya kuwa na maisha ya kikawaida yanayoridhisha, kwa sababu ya matatizo aina kwa aina ya maisha wanaokabiliwia nayo kila siku. Alisema UM unasubiri, kwa hamu kuu, kushirikiana kikazi na Stevie Wonder kwa makusudio ya kuendeleza haki na hali njema ya walemavu na wale waliokosa uwezo. Kadhalika, KM alimwomba Stevie Wonder kutafakaria kidhati ile rai ya yeye kuimba wimbo wake mmoja maarufu unaoitwa "Signed, sealed and delivered" yaani "Imeshasahihiwa, kupigwa mhuri na tayari kutekelezwa", kwa madhumuni ya kuwahamasisha wajumbe wa kimataifa watakaohudhuria Mkutano Mkuu wa UM juu ya Udhibiti Bora wa Taathira za Mabadiliko ya Hali ya Hewa, utakaofanyika kuanzia wiki ijayo, kwenye mji wa Copenhagen, Denmark nao vile vile kufikia itifaki ya pamoja, itakaotiwa sahihi na kutekelezwa kimataifa katika kudhibiti madhara yanayoletwa na uharibifu wa hali ya hewa na mazingira.