Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkurugenzi Mkuu mpya wa IAEA aanza kazi rasmi Vienna

Mkurugenzi Mkuu mpya wa IAEA aanza kazi rasmi Vienna

Yukiya Amano, Mkurugenzi Mkuu mpya wa Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) ameanza kazi rasmi, hii leo, Ijumanne mjini Vienna. Kwenye taarifa kwa waandishi habari ameeleza ya kuwa "mazingira yaliozikabili shughuli za taasisi yao kwa sasa ni ya zahma tupu."

Mkurugenzi Amano alieleza Shirika la IAEA limekabiliwa na masuala magumu" kadha wa kadha, na atajaribu, kwa uwezo wake, kusaidia kuyatatua masuala haya kwa utaratibu unaofaa, hasa yale masuala yanayojumlisha uzuiaji wa uenezaji wa silaha za kinyuklia, maamirisho ya usalama wa huduma za kinyuklia, taratibu za kukidhi mahitaji ya nishati kwa kutumia viwanda vya kinyuklia, na uwezekano wa kudhibiti bora teknolojiya ya nyuklia kwenye uangalizi wa afya, na pia usimamizi unaofaa katika kudhibiti rasilmali ya maji. Aliahidi kwamba, yeye binafsi, atajitahidi kuyatekeleza majukumu yake bila ya upendeleo na kwa kutegemewa, kwa uwiano na wadhifa wa kitaaluma alionao. Aliyaomba Mataifa Wanachama yote kumsaidia katika kuyakamilisha maadili hayo kikazi.