Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

'Siku ya Ukimwi Duniani', UM kuhimiza mataifa kufuta sheria za kibaguzi dhidi ya waathirika wa VVU

'Siku ya Ukimwi Duniani', UM kuhimiza mataifa kufuta sheria za kibaguzi dhidi ya waathirika wa VVU

UM unaiadhimisha tarehe ya leo kuwa ni Siku ya UKIMWI Duniani. Mada ya taadhima za mwaka huu inatilia mkazo Upatikanaji wa Haki za Binadamu kwa Wote.

Jumuiya ya Mashirika ya UM Dhidi ya UKIMWI (UNAIDS) imetangaza mwito maalumu kwa siku hii, unaozihimiza nchi zote wanachama katika UM, kufuta zile kanuni zenye kuwatenga na kuwabagua watu waliopatwa na UKIMWI. UM umechapisha ripoti maalumu iliowasilishwa siku ya leo yenye muktadha usemao Watoto na UKIMWI: Ripoti ya Nne Kutathminia UKIMWI kwa 2009. Ripoti imeeleza kwamba juhudi za kitaifa kupambana na UKIMWI, hususan katika kuzuia maambukizo ya virusi vya maradhi, kwa mtoto kutoka mama mjamzito, juhudi hizi zimeonyesha mafanikio ya kutia moyo mwaka huu, katika nchi nyingi ulimwenguni. Lakini hata hivyo, ripoti ilitilia mkazo, watoto wengi walioathirika na VVU na UKIMWI bado wanaendelea kusumbuliwa na matatizo ya kutekelezewa huduma za kimsingi, kwa ujumla. Ripoti ilitayarishwa bia na mashirika manne ya UM, yakijumlisha Shirika juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), UNAIDS, Shirika la UM juu ya Udhibiti wa Idadi ya Watu (UNFPA) na Shirika la Afya Duniani (WHO). Ripoti ilikusanyisha takwimu zenye kubainisha msaada wanaopata wanawake na watoto katika kujikinga na maambukizo ya VVU, na iliorodhesha kanuni za kuongoza mataifa kuchukua hatua za haraka ili kudhibiti mapema janga la UKIMWI kimataifa.