Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugonjwa maututi wa sotoka, uliodhuru wakulima miaka iliopita, unakaribia kufyekwa kimataifa

Ugonjwa maututi wa sotoka, uliodhuru wakulima miaka iliopita, unakaribia kufyekwa kimataifa

Imetangazwa kutoka Roma, Utaliana, leo hii, yalipo Makao Makuu ya Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) ya kuwa jamii ya kimataifa inakaribia kufyeka milele lile janga maututi la maradhi ya sotoka, ugonjwa wa kuhara wenye kuambukiza ng\'ombe, maradhi ambayo kwa muda wa miaka mingi, yalikuwa yakiwasumbua wakulima, hasa kwenye yale maeneo ya Afrika, kusini ya Sahara.

Shirika la FAO, likijumuika na Shirika la Dunia Kudhibiti Afya ya Mnyama [wa Kufuga] au Shirika la OIE, pamoja na wadau wengine, wanatarajiwa kutangaza rasmi, mnamo miezi 18 ijayo, kwamba ugonjwa mbaya wa sotoka, wenye kuangamiza wanyama, utakuwa umekomeshwa na kufyekwa kimataifa. Tukio hili la kihistoria, katika mazingira ya afya ya wanyama, linalinganishwa sawa na kutua kwenye mwezi kwa roketi ya Apollo 11. Hii itakuwa ni mara ya kwanza katika historia, kwa binadamu kufanikiwa kukomesha ugonjwa wa mnyama, na ni mara ya pili ugonjwa huwa umetupwa kwenye kapu la kihistoria kimataifa, kutokana na juhudi za wanadamu, ugonjwa wa kwanza kufanywa hiyvo, ulikuwa ni maradhi ya ndui.