Mashirika ya UM yamehadharisha kuhusu tofani Bukini
Mashirika ya UM yametangaza kuwa na wasiwasi juu ya kunyemelea kwa majira ya matofani na vimbunga katika taifa la Bukini, maafa ambayo kama hayajadhibitiwa yanaashiriwa huenda yakaathiri maisha ya watu 600,000.
Utabiri wa hali ya hewa unabashiria Bukini huenda ikavamiwa na dhoruba za matofani makali kwenye majira yajayo, maafa yenye uwezo wa kugharikisha maisha, na pia kunyima watu uwezo wa kujipatia rizki, na vile vile kuharibu kwa kiwango kikubwa, miundombinu ya nchi. Kwa hivyo, mashirika ya kimataifa yanayohudumia misaada ya kiutu yametoa mwito wa kutaka yafadhiliwe mchango wa dola milioni 6 kutayarisha mahitaji halisi kwa ule umma unaoishi kwenye maeneo yanayohatarishwa na maafa ya vimbunga. Mashirika ya kimataifa yanahitajia pia maturubali, madawa, tembe za kusafishia maji na vifaa vya tiba ya afya, maskuli na pia vifaa vya burudani.