Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Alkhamisi KM Ban Ki-moon anatazamiwa kusafiri kwenda Trinidad na Tobago kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Serikali Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM). Kwenye ziara hiyo, itakayochukua siku tatu, KM anatarajiwa kuwahimiza viongozi wa CHOGM kuhudhuria Mkutano Mkuu juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa wa Copenhagen, utakaofanyika mwezi ujao, kikao ambacho kinaandaliwa kujaribu kukamilisha mapatano ya kuanzisha mkataba mpya wa kudhibiti bora athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Wakuu wa kiserikali watanasihiwa na KM kuwa na mtazamo halisi utakaowawezesha kufikia mapatano yanayoridhisha kwenye Mkutano Mkuu wa Copenhagen, maafikiano yatakayodumishwa, yenye usawa na yanayotimiza matakwa ya kisayansi.

Hali ya kiutu katika Ufilipina imeripotiwa kwa sasa kuwa ni ya hatari sana, hususan kwa umma uliong'olewa makazi kutokana na tofani kali iliopiga huko katika siku za karibuni, na huathiri zaidi wale raia walionasa kwenye vijiji vilivyozama na vyenye shida kuu kuvifikia. Ofisi ya Misaada ya Dharura ya UM (OCHA) imeripoti nyumba 46,000 ziliangamizwa kikamilifu, wakati nyumba nyengine 261,000 ziliharibiwa kwa sehemu. Mnamo tarehe 16 Novemba (2009), karibu familia 79,000 - zinazojumlisha watu 382,000 ziada - zimeripotiwa bado kuishi kwenye vijiji 871 vilivyofurika, raia ambao wanakabiliwa na matatizo ya kihali yanayoambatana na ukosefu wa maji safi na salama, mazingira safi na vifaa vya kumudu afya, hasa kwenye kambi za makazi ya muda. Mashirika ya UM yanajitahidi hivi sasa, kwa kulingana na hali ilivyo, kuhudumia misaada ya kihali kwa waathirika hawa wa tofani katika Ufilipina.