Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Kwenye maelezo ya tamko la KM juu ya mauaji ya kikatili ya raia 40 ziada, yaliotukia juzi kwenye jimbo la Maguindanao, Ufilipina ya Kusini, Ban Ki-moon alishtumu vikali jinai hii ya kutisha, uhalifu ambao alisema ulioripotiwa kufungamana na kampeni ya uchaguzi wa serikali ya majimbo.

KM aliwatumia mkono wa pole kwa aila zote za waathirika wa tukio hilo, na alitumai kutachukuliwa kila hatua na wenye madaraka, kuhakikisha wakosa wanashikwa na kufikishwa mahkamani kukabili haki.

Ujumbe maalumu unaowakilisha Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika (UA) umeanza ziara rasmi ya siku tatu nchini Sudan, kutokea Darfur Kaskazini, ambapo walikutana na maofisa wa Serikali ya jimbo, pamoja na viongozi wa kijamii na watumishi wa UNAMID. Ujumbe wa UA unaoongozwa na Balozi Joseph Nsengimana wa Rwanda, na uliwasili kwenye mji wa El Fasher Ijumanne, kupata tathmini binafsi kuhusu hali ya usalama kwenye eneo la vurugu, na walijadiliana pia na watumishi wa UNAMID kuhusu operesheni zao.

Msemaji wa KM, akijibu suala kwenye mahojiano ya mchana na waandishi habari wa kimataifa katika Makao Makuu, kuhusu eneo la mvutano baina ya Nigeria na Cameroon la Rasi Bakassi, alisema Waangalizi Raia wa UM waliopo kwenye eneo husika wanawasiliana kwa ukaribu zaidi kwenye kazi zao na Serikali ya Jimbo la Cross River katika Nigeria, kuhusu hali ya watu waliohamishwa makazi kutoka Bakassi, baada ya itifaki ya kulirejesha eneo la mvutano kwa Cameroon. UM unahusiana na Nigeria na Cameroon kwenye shughuli zake, kwa kulingana na mapendekezo ya mfumo wa Kamati ya Kufuatilia, ili kuhakikisha Mapatano ya Greentree yanaendelea kutekelezwa kama inavyotakikana kisheria na makundi yote husika na itifaki hiyo.

Abdalmahmood Abdalhaleem, Mwakilishi wa Kudumu wa Sudan katika UM amenakiliwa kuilaumu vikali fafanuzi ya ripoti mpya ya KM kuhusu hali katika jimbo la mtafaruku la Darfur. Alisema ripoti ya KM ilikosa matumaini, na anaamini wakati umeshawadia kwa vikosi vya ulinzi amani vya UM kujitayarisha kuihama Sudan. Alisisitiza ripoti ilisahau kujumlisha taarifa muhimu juu ya mchango wa Khartoum, uliowasaidia wanajeshi wa kimataifa kuenezwa kwenye maeneo ya vurugu bila ya matatizo. Msemaji wa KM alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Balozi wa Sudan, alisisitiza mashirika mawili ya UM yaliopo Sudan - yaani shirika la kulinda amani kwa Darfur, UNAMID, na taasisi ya kusimamia utulivu kwenye eneo la Sudan Kusini, UNMIS - yalianzishwa nchini kwa kulingana na madaraka ya Baraza la Usalama, na mabadiliko yoyote kuhusu kazi za mashirika hayo ya UM yatategemea uamuzi wa Baraza.