Skip to main content

Urajisi wa wapiganaji wa zamani waanzishwa rasmi katika Darfur

Urajisi wa wapiganaji wa zamani waanzishwa rasmi katika Darfur

Vile vile kuhusu Sudan, mnamo siku ya leo, katika mji wa El fasher, wapiganaji wa zamani 5000 kutoka makundi kadha yaliotia sahihi Mapatano ya Amani kwa Darfur, wameanza urajisi wa kujumuishwa kwenye maisha ya kawaida nchini.

Kwa mfano, waliokuwa wapiganaji 400 kutoka Darfur Kaskazini, wanatazamiwa kusajiliwa kwenye mji wa El Fasher, kwenye mradi utakaochukuwa siku tatu, utaratibu ambao baadaye utahamishiwa kwenye mji wa Nyala, Darfur Kusini, na kufuatiwa na Darfur Magharibi. Mfumo huu wa usajili wa wapiganaji wa zamani, unajumuisha kadhia ya kuwapatia mafunzo waliokuwa wapiganaji, yatakayowasaidia kujiunganisha vizuri zaidi na maisha ya kikawaida kwenye jamii zao, na kuhakikisha uhalisi wa nyaraka walizonazo ili kurahisisha huduma za utawala, na baadaye kuwafanyia wapiganaji uchunguzi wa magonjwa na ulemavu, na pia kuchukuwa alama zao za vidole na, hatimaye, kuwapatia vitambulisho. Kadhalika, wapiganaji wanoishiriki kwenye utaratibu huu watafadhiliwa posho ya fedha za kienyeji sawa na dola 150, na baada ya miezi miwili watapatiwa vocha ya kuhudumia chakula na shughuli nyenginezo za msingi ili kuendesha maisha ya kikawaida.