Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ripoti mpya ya Shirika la UM juu ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) leo imeripoti ya kuwa idadi ya watafiti na wachunguzi wa kitaaluma katika mataifa yanayoendelea imeongezeka, kwa kiwango cha kutia moyo katika miaka ya karibuni. Ripoti ilieleza baina ya miaka ya 2002 hadi 2007, idadi ya watafiti katika nchi zinazoendelea ilizidi kwa asilimia 56, ikimaanisha nchi nyingi zenye uchumi haba zimetambua umuhimu wa kuendeleza tafiti zinazowasilisha ubunifu unaoleta mageuzi ya kiteknolojia kwenye maendeleo yao.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imechapisha ripoti mpya kuhusu uhuru wa watu kutembea na fursa ya kufikia sehemu mbalimbali za eneo liliokaliwa kimabavu la Ufukwe wa Magharibi ya Mto Jordan. Kwa mujibu wa ripoti, mnamo miezi sita iliopita, walowezi Waisraili wenye madaraka ya kimabavu katika eneo la Ufukwe wa Magharibi ya Mto Jordan, wameruhusu kidogo kwa WaFalastina kwenda watakapo baina ya vituo vya miji ya WaFalastina kwenye eneo. Lakini katika kipindi hicho hicho, ripoti ilibainisha kuwepo ukosefu wa maendeleo muhimu juu ya uwezo wa WaFalastina kufikia sehemu kadha za ardhi katika Magharibi ya Ufukwe wa Mto Jordan. Kwa mfano, sehemu moja maalumu, iliokaliwa kimabavu katika Magharibi ya Mto Jordan, WaFalastina hawaruhusiwi kuitumia wala kuihudumia kimaendeleo, sehemu ambayo hujumlisha asilimia 60 ya ardhi yote ya WaFalastina ilionyakuliwa na watawala wa Israel.

Kadhalika, mnamo Ijumatatu ya leo, UM umechapisha ripoti mpya kuhusu namna maazimio ya Baraza la Usalama yanavyotekelezwa na Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) kwenye maeneo ya operesheni zao, kati ya kipindi cha baina ya miezi ya Julai mpaka Oktoba 2009. Ripoti ilizingatia maendeleo kwenye miradi ya kisiasa, masuala ya kudhibiti utulivu na usalama, ikichanganyika na hali kuhusu huduma za kiutu katika Darfur. Ndani ya ripoti KM alieleza, ijapokuwa UNAMID inaendelea kujihusisha kwenye majukumu muhimu ya kulinda raia, na kurahisisha huduma za kupeleka misaada ya kiutu kwenye maeneo wanamoishi umma ulioathirika na mgogoro wa Darfur, huduma za UNAMID bado huzorotishwa na matatizo kadha mengine, yakijumlisha pia matishio kwa watumishi wa kimataifa wanofanya kazi Darfur, hatari inayoletwa na uhasama na mapigano baina ya Chad na Sudan, na kwenye Darfur yenyewe, pamoja na ukosefu wa suluhu ya jumla juu ya mgogoro wa Darfur.

Tangu tarehe 14 Novemba 2009, Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) na mashirika wenzi yanayohudumia misaada ya kiutu katika Yemen, yalifanikiwa kugawa tani za metriki 2,065 za chakula kwa watu muhitaji 100,000 walioathirika na mapigano; na ugawaji wa chakula kwa duru ya mwezi Novemba unatazamiwa kukamilishwa katika wilaya zote husika katika siku za karibuni, kabla ya Siku Kuu ya Eid kuadhimishwa kwenye mwisho wa wiki. Wakati huo huo, kuanzia Ijumatatu iliopita, Ofisi ya UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) ilipeleka misaada ya kimsingi iliofadhiliwa aila 5,000 ziliopo kwenye majimbo matatu ya Yemen kaskazini. Misaada ya maji ya kunywa na maji ya matumizi, yalio safi na salama, inaendelea kupelekewa wahamiaji waliopo sehemu ya Al Marzak, kwenye Jimbo la Hajjah. Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) lilituma matangi ya maji ziada kwenye kambi mpya za wahamiaji wa ndani, na kwenye kambi nne nyengine nje ya eneo hilo, wakati zile huduma za kufuatilia ugawaji bora wa misaada ya kihali, kama maji safi na huduma za kuua vidudu bado zinaendelewa bila kusita kwenye eneo. Wakati huo huo, mashirika ya Oxfam na UNICEF yamemaliza kujenga vyoo 900 kutumiwa na wahamiaji wa kambi za Al Marzak.

Asubuhi Baraza la Usalama lilikutana kujadilia hali katika Bosnia na Herzegovina. Valentin Inzko, Mjumbe Mkuu wa UM kwa Bosnia na Herzegovina aliwaambia wajumbe wa mataifa 15 wanachama katika Baraza la Usalama kwamba hali ya kutoafikiana imejiri kwenye mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kudumisha amani ya eneo hilo, kwa sababu ya utatizi wa aina mbili: awali, utatizi wa ile sehemu inayojigamba kuwa Republika Srpska na mfumo wake wa kimamlaka, kijumla; na pili, utatizi umejiri kwenye ufahamivu wa masuala muhimu yanayotakikana kushughulikiwa na vitengo vyote viwili vya kisiasa, kuhusu mfumo halisi wa Kitaifa katika Bosnia na Herzegovina.