Skip to main content

Mazungumzo ya Redio ya UM na mshindi wa mashindano ya picha ya UNDP/Olympus/AFP kutoka Kenya

Mazungumzo ya Redio ya UM na mshindi wa mashindano ya picha ya UNDP/Olympus/AFP kutoka Kenya

Ijumatano raia wawili wa kutoka Kenya, pamoja na mzalendo mwanamke kutoka Morocco, walitunukiwa zawadi maalumu, kwa picha zao zilizoonyesha namna watu wa kawaida barani Afrika, wanavyoshiriki kwenye harakati za kutunza na kuhifadhi mazingira - ikijumlisha zile shughuli za kupandisha miti, na huduma za kuigeuza mifuko ya plastiki, iliotupwa kwenye majaa baada ya kutumiwa, kuwa mikoba ya pochi na vikapu, ikiwa miongoni mwa kadhia muhimu zinazochangia kimataifa katika kupunguza athari haribifu za mabadiliko ya hali ya hewa.

Mkuu wa UNDP, Helen Clark, kwenye tafrija ya kuzawadia tunzo kwa washindi wa upigaji picha, iliofanyika kwenye jiji la New York, alinakiliwa akisema "kwa washindi kufanikiwa kuonyesha kwenye picha zao taswira zinazofafanua mchango wa raia wa kawaida barani Afrika, katika kupambana na uharibifu wa hali ya hewa, ni kadhia inayotuwezesha kuthibitisha na kushuhudia nguvu, zisio za kawaida, za picha katika kusimulia hadithi za kutia moyo juu ya hifadhi ya mazingira." Shirika la UNDP lilianzisha mashindano haya ya picha kwa ushirikiano na watengenezaji kamera wa Shirika la Biashara la Olympus, lenye Makao Makuu mjini Tokyo, Ujapani pamoja na Taasisi ya Shirika la Habari la Kifaransa (AFP).

Mtayarishaji wa vipindi vya Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya UM, AZR, alipata nafasi ya kufanya mahojiano na mmoja wa washindi aliyepata zawadi ya kwanza, kutoka Kenya, anayeitwa Simon Ndegwa.

Sikiliza mahojiano kamili kwenye idhaa ya mtandao.