Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulio ya chuki za wageni Afrika Kusini yamelaaniwa na UNHCR

Mashambulio ya chuki za wageni Afrika Kusini yamelaaniwa na UNHCR

Mashambulio yaliotukia Ijumanne kwenye eneo la De Doorns, Afrika Kusini yaliochochewa na chuki na hofu dhidi ya wageni wa nchi, ikijumlisha raia wa Zimbabwe wenye kuomba hifadhi ya kisiasa, yaliripotiwa kusababisha baadhi ya wahamiaji 3,000 kukimibia mabanda waliokuwa wakijistiria ili kunusuru maisha, na ni kitendo ambacho kililaaniwa na Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR).

Kwa mujibu wa msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Andrej Mahecic, mashambulio yalifanyika kwenye shamba la mizabibu, liliopo kilomita 140, kaskazini-mashariki ya mji wa Cape Town, ambapo pia huishi jamii ya wazalendo wa Afrika Kusini 13,000. Hivi sasa watumishi wa UNHCR wanajaribu kuwasaidia waathirika wa mashambulio ambao wanasubiri matokeo ya majadiliano na jamii ya wakulima waliowashambulia mwanzo wa wiki, wakulima waliowatuhumu wageni kuwa wanawaibia ajira kwa kukubali kufanya kazi kwa mishahara midogo kwenye mashamba ya mizabibu. Shirika la UNHCR limekumbusha kwamba wahamiaji waliosajiliwa rasmi, pamoja na wale wageni walioomba hifadhi ya kisiasa, wote wana haki ya kufanya kazi nchini Afrika Kusini, licha ya kuwa kuna mvutano na hali ya wasiwasi ambayo husababisha miripuko ya vurugu la mara kwa mara baina yao na wenyeji wazalendo.