Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Benki Kuu ya Dunia inasisitiza miundombinu dhaifu ya Afrika inahitajia misaada maridhawa kukuza maendeleo

Benki Kuu ya Dunia inasisitiza miundombinu dhaifu ya Afrika inahitajia misaada maridhawa kukuza maendeleo

Kwenye ripoti ya utafiti wa Benki Kuu ya Dunia kuhusu hali ya miundombinu katika Afrika, imeripotiwa kwamba mnamo miaka michache iliopita, bara la Afrika lilifaidika kujipatia maendeleo muhimu.

Ripoti iliopewa mada isemayo Miundombinu ya Afrika: Wakati wa Mabadiliko Umewadia, imeeleza ya kuwa kuanzia 2006 asilimia 50 ziada ya idadi ya watu katika Afrika wanaishi kwenye maeneo yanayowawezesha kupokea ishara ya kuwasiliana kwa kutumia simu za mkononi. Kadhalika nchi tano katika Afrika zimeshakamilisha lile lengo la maendeleo ya milenia la kuwawezesha raia wao wote kupata maji safi na salama, wakati nchi 12 nyenginezo zipo kwenye mkondo wa kutekeleza huduma hiyo kwa umma. Hata hivyo, ripoti ya Benki Kuu ya Dunia imehadharisha ya kuwa kutokana na hali dhaifu ya miundombinu katika zile nchi za Afrika ziliopo kusini ya Sahara, mazingira haya yameonekana kumega na kudhuru asilimia mbili ya ongezeko la uchumi wa taifa kila mwaka na kupunguza uzalishaji kwa asilimia 40 - hali ambayo huathiri ugawaji wa umeme, maji safi, maamirisho ya barabara za usafiri usio matatizo na kwenye usambazaji wa taarifa za kisasa pamoja na matumizi ya teknolojia ya mawasiliano ya kisiku hizi. Ripoti ya Benki Kuu inajumlisha matokeo ya tathmini ya kina juu ya hali ya miundombinu iliofanyika katika nchi 24 zilizotapakaa katika sehemu mbalimbali za Afrika.