UNICEF inaunga mkono utekelezaji wa Mkataba wa Haki ya Mtoto kimataifa

19 Novemba 2009

Philip O\'Brien, Mkurugenzi wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) anayehusika na Uchangishaji Pesa na Mashirkiano aliwaambia waandishi habari Geneva Alkhamisi ya leo,

kwamba nchi 70 kati ya 193 zilizotia sahihi na kuridhia Mkataba juu ya Haki ya Mtoto zimefanya marekibisho muhimu kwa kuweka mifumo na taratibu zilizokubalika kuhusu haki za watoto kwenye kanuni zao za kitaifa. Alisema Mkataba ulihamasisha athari za moja kwa moja zilizokuwa na natija za kutia moyo kwenye maendeleo ya watoto. Mathalan, kwa kulingana na mapendekezo ya Mkataba juu ya Haki ya Mtoto, nchi zilizoridhia chombo hiki cha sheria ya kimataifa zilifanikiwa kupunguza, kwa idadi kubwa kabisa idadi ya watoto waliokuwa wakifariki kila siku bila ya lazima, na wala sababu. Katika 1990, takwimu za UM zilionyesha watoto milioni 12.5 walikuwa wakifariki ulimwenguni kila mwaka kabla ya kutimia umri wa miaka mitano. Lakini katika 2008 jumla ya watoto wanaofariki kila mwaka kabla ya kufika miaka mitano iliteremka na kufika watoto milioni 9, mwelekeo ambao badao unaendelea na kushika kasi, kwa mujibu wa taarifa ya UNICEF.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud