Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon amemtumia salamu za pongezi Raisi Hamid Karzai wa Afghanistan baada ya kuapishwa Alkhamisi, kuwa Raisi atakayetumikia awamu ya pili ya utawala, kufuatia uchaguzi uliofanyika nchini katika wiki za karibuni. KM aliunga mkono ahadi za Raisi Karzai za kutumikia raia wote WaAfghani, na kupiga vita vitendo vya rushwa, na katika kuimarisha utawala bora, na pia kuhakikisha hali ya usalama inajiri nchini, na kwamba atajitahidi kuhudumia mahitaji ya taifa, kwa ujumla, kwa kulingana na fafanuzi alizowakilisha kwenye hotuba yake ya kutawazishwa uraisi. KM alisema UM utaendelea kushirikiana na Raisi Karzai na serikali yake, pamoja na umma wa Afghanistan na washirika wa kimataifa katika huduma za maendeleo ya kukuza uchumi na jamii nchini mwao.

Wajumbe wa Baraza la Usalama walikutana asubuhi kushauriana juu ya taarifa mpya ya kazi za Kamati ya Vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Umma wa Korea (DPRK), inayosimamiwa na Uturuki. Kadhalika, Baraza la Usalama leo lilipata fursa ya kusikiliza ripoti ya Edmond Mulet, KM Msaidizi kwenye Masuala ya ya Operesheni za Ulinzi Amani kuhusu hali katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK).

Radhika Coomaraswamy, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Watoto Walionaswa Kwenye Mapigano ya Kijeshi ameripotiwa kuhitimisha ziara ya siku mbili katika Darfur Alkhamisi ya leo, ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku kumi anayofanya nchini Sudan ambayo ataikamilisha Ijumatatu, tarehe 23 Novemba 2009. Alipokuwepo Darfur, Coomaraswamy alikutana na wadau mbalimbali wanaohusika na mpango wa amani katika El Fasher, Darfur Kaskazini na El Geneina, Darfur Kusini, wakijumlisha Mawali/Magavana wa majimbo hayo mawili. Vile vile alikutana na viongozi wa jamii na kidini na makundi ya wahamiaji wa ndani ya nchi waliohajiri makwao kwa sababu ya uhasama. Alisema aliridhika na zile bidii za kuanzisha taasisi za kufuatilia na kukabili matatizo ya kuajiri, kusio halali, kwa wapiganaji watoto, masuala ya udhalilishaji wa kijinsia na matumizi ya mabavu dhidi ya watoto wadogo. Aliwasihi viongozi wa kidini kuamsha hisia za jamii ziliopo kwenye majimbo yao kuhusu masuala haya yanayokiuka haki za watoto.

Shirika la Ulinzi Amani la UM katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na Chad (MINURCAT) limeripoti wanajeshi 42 wa kutoka Cambodia wamewasili katika mji wa Abeche - ambapo wanatazamiwa kusaidia katika udhibiti wa usafirishaji mali za UM na watumishi wa kimataifa waliopo huko. Kuwasili kwa vikosi vya Cambodia kunajumlisha wanajeshi 2,749 wa MINURCAT, ikiwakilisha asilimia 52.61 ya uwezo unaohitajika kudhibiti shughuli za kuimarisha amani kwenye eneo hili. MINURCAT ilieleza kwamba wanajeshi wa Cambodia wanashiriki, kwa mara ya pili, kwenye shughuli za kulinda amani za UM, baada ya kusaidia kwenye kadhia muhimu ya kufyeka mabombu yaliotegwa ardhini katika Sudan mnamo 2006.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti ya kuwa mapigano sasa yameingia wiki ya tatu tangu operesheni za kijeshi ziliposhitadi kwenye jimbo la Pakistan la Waziristan Kusini. Ripoti ya OCHA imebainisha watu 400,000 waililazimika kukimbia maeneo yao na kuomba hifadhi kwenye wilaya mbili jirani. Kuhusu wahamiaji waliosajiliwa na UM, iliripotiwa watu 300,000 walihajiri makwao kuanzia katikati ya mwezi Oktoba, na fungu kubwa la umma huu hujumlisha watu masikini wanaohitajia kidharura kufadhiliwa misaada ya kihali kunusuru maisha.Watumishi wa kimataifa wanaohudumia misaada ya kiutu waliopo kwenye eneo la uhasama la Waziristan Kusini, bado wanaendelea na shughuli za kuhudumia misaada ya kunusuru maisha ya mamia elfu ya wahamiaji wa ndani ya nchi, licha ya kuwa hali ya amani bado haiaminiki.