Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNIDO asema 'maendeleo ya viwanda ndio ufunguo wa kuiunganisha Afrika na uchumi wa dunia'

Mkuu wa UNIDO asema 'maendeleo ya viwanda ndio ufunguo wa kuiunganisha Afrika na uchumi wa dunia'

Kandeh K. Yumkella, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) amesihi kwamba bara la Afrika linahitajia kudhibiti vizingiti vya kiuchumi vinavyokwamisha maendeleo yao, kwa kukuza uzalishaji wa viwandani, hatua ambayo ikitekelezwa alisema huenda ikamegea Afrika sehemu kubwa zaidi ya natija za kiuchumi kutoka soko la kimataifa, na kunufaisha uchumi mzima wa ulimwengu wetu.

Yumkella alisema licha ya kuwa katika kipindi cha baina ya miaka ya 2003 mpaka 2007, maendeleo ya viwandani katika Afrika yalikuwa polepole, kwa kiwango cha kutia moyo cha asilimia sita kila mwaka, hata hivyo ongezeko hili, alisisitiza halikufanikiwa kuondosha vizingiti vyengine kadha vinavyoathiri uwezo wa makarkhana ya Afrika kuendeleza ile sekta ya kutengenezea bidhaa. Alisema vizingiti hivi ni lazima vishughulikiwe kidharura. Risala hii ya Mkuu wa UNIDO ilitangazwa kabla ya tarehe 20 Novemba, siku ambayo huadhimishwa na UM kuwa ni Siku ya Viwanda kwa Afrika. Miongoni mwa vizuio vinavyozorotisha maendeleo ya viwanda barani Afrika hujumlisha ujuzi mdogo wa shughuli za viwanda na uwezo haba wa kiufundi, ikichanganyika na ukosefu wa misaada kutoka taasisi za kitaifa, mchango mdogo sana wa fedha kuhudumia viwanda na pia soko dhaifu la eneo kuuzia bidhaa zao. Alitilia mkazo ya kuwa matatizo ya kifedha na uchumi katika dunia, vile vile yalichafua utaratibu wa Afrika kukuza maendeleo ya viwanda. Juu ya hayo, Mkurugenzi wa UNIDO alisema bara la Afrika litaweza kufaidika na biashara ya kimataifa pindi "litatumia shughuli za viwandani kuwa kama ni injini ya kukuza uchumi na maendeleo" kwenye eneo.