Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Mkutano Mkuu wa UM wa kuzingatia maendeleo kwenye bidii za pamoja katika kudhibiti bora akiba ya chakula duniani, uliofanyika Roma, Utaliana kwa siku tatu, ulihitimisha majadiliano Ijumatano bila ya wajumbe wa kimataifa kukubaliana juu ya mchango wa fedha maridhawa zinazohitajika kupambana na tatizo kuu la njaa katika ulimwengu. Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) - liliotayarisha mkutano - limekadiria mchango wa dola bilioni 44 utahitajika kidharura, kuwekezwa kila mwaka, kwenye kilimo, kupiga vita, kwa mafanikio, matatizo ya njaa duniani.

KM Ban Ki-moon ametangaza kusikitishwa na uamuzi wa Serikali ya Israel wa kupanua maeneo ya makazi ya walowezi ya Gilo, yaliojengwa kwenye ardhi ya WasFalastina iliokaliwa kimabavu, kufuatia mapigano ya 1967. Taarifa iliotolewa na Ofisi ya Msemaji wa KM ilieleza kwamba KM amekariri tena kwamba makazi ya walowezi kwenye maneo ya WaFalastina, ni kitendo kisiokubalika na sheria ya kimataifa, na ametoa mwito wenye kuisihi Israel kuhishimu ahadi iliotoa, chini ya mapatano ya Ramani ya Amani juu ya Mzozo wa Mashariki ya Kati, na kuitaka isitishe, haraka, shughuli zote za ujenzi kwenye makazi ya walowezi, ikijumlisha kile kinachodaiwa kama ‘upanuzi maumbile' wa jamii za walowezi. Alisisitiza KM vitendo hivi vya Israel vinadhoofisha na kuchafua bidii za jamii ya kimataifa za kuleta amani, na huzusha mashaka juu ya uwezekano wa kuwa na suluhu ya Mataifa-mawili jirani ya Falastina na Israel, yatakayoishi pamoja kwa amani. Ijumanne Israel iliripoti rasmi kuwa itapanua makazi ya walowezi yaliopo kwenye wilaya ya Mayahudi ya mji wa Jeruslaem, ndani ya eneo la WaFalastina liliotekwa kwenye vita vya 1967.

Ofisi ya UM juu ya Uratibu wa Masuala ya Kiutu/Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imetangaza ombi la kutaka ifadhiliwe msaada wa jumla, wa dola milioni 470, kutumiwa kwenye miradi 74 katika 2010 katika Chad. Michele Falavigna, Mratibu wa Misaada ya Kiutu kwa Chad, aliwaambia waandishi habari Geneva msaada huo utajumlisha fedha zinazotakikana kuhudumia mahitaji ya kiutu kwa taifa zima la Chad, na hautotumiwa kwenye eneo la uhasama pekee la Chad Mashariki, kama ilivyokuwa ikifanyika siku za nyuma. Alitumai mchango huo wa kimataifa ukitekelezwa utaiwezesha UM kuendeleza huduma za kunusuru maisha kwa wahamiaji wa kutoka nchi jirani, na wale wahamiaji wa ndani ya nchi waliong'olewa makazi kwa sababu ya kuzuka uhasama kwenye maeneo yao, hatua ambayo itasaidia kuwasilisha suluhu ya kuridhisha kwenye mzozo wa Chad.

Ofisi ya UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) imeripoti kushuhudia muongezeko mkubwa wa wahamaji wa kutoka Afrika, wanaoelekea nchi za Amerika ya Latina, kufuatia uamuzi wa nchi za Ulaya kubana fursa ya watu kuingia kwenye maeneo yao. Ripoti ilieleza baadhi ya wahamiaji wa Afrika huelekea mataifa ya Mexico na Guatemala, ambayo huyatumia kama hatua ya mwanzo ya kuelekea Marekani, wakati makundi mengine ya wahamiaji huamua kuelekea bandari za Argentina na Brazil. Wahamiaji wa Afrika nchini Brazil sasa hivi wanajumlisha kundi kubwa la wageni, sawa na asilimia 65 ya wahamiaji wote waliosajiliwa kuomba hifadhi ya kisiasa nchini humo, kwa mujibu wa taarifa ya kamati ya taifa ya Brazil juu ya wahamiaji wageni. Kuhusu Argentina, iliripotiwa wahamiaji wa kutoka Afrika 3,000 wamesajiliwa kuishi nchini humo hivi sasa, wakati miaka minane iliopita jumla ya wahamiaji wa Afrika katika ilikuwa ni darzeni chache tu. UNHCR imeripoti idadi ya waombaji hifadhi ya kisiasa nchini Argentina imeongezeka kwa ghafla katika kipindi cha karibuni, na wahamiaji takriban 1,000 husajiliwa kuingia nchini kila mwaka, na thuluthi moja ya wahamaji hawa hujumuisha wale waliohajiri kutoka nchi za Afrika.

Wajumbe wa Bodi la Uchunguzi juu ya ukweli, na mazingira yaliosababisha mauaji ya Benazir Bhutto, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan wamekiri kuwa walikutana karibuni na Raisi Mstaafu wa Pakistan, Pervez Musharraf. Walisema walikuwa na mazungumzo ya kweli, yenye uwazi na ya kuhishimiana na kiongozi huyo. Kwa mujibu wa taarifa ya wawakilishi wa Bodi la Uchunguzi, Raisi mstaafu Musharraf aliulizwa masuala mengi yanayohusiana na kiini cha upelelezi wao. Kadhalika wajumbe wa tume walikutana na darzeni kadha za watu wengine, ili kukusanya ushahidi utakaowasaidia kuendesha kazi zao kama walivyoamrishwa na Baraza la Usalama.

Ijumatano asubuhi, Baraza la Usalama lilipitisha azimio kuhusu Bosnia na Herzegovina. Kwenye azimio, Baraza la Usalama limeidhinisha kuongeza muda wa vikosi vya kimataifa vya kusawazisha utulivu na amani katika Bosnia na Herzegovina kwa mwaka mmoja zaidi, vikosi ambavyo hujulikana kama majeshi ya EUFOR.