Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) limeripoti ya kuwa miradi mingi isiochafua hewa, na inayotumia nishati inayotunza mazingira, inalengwa sasa hivi kutekelezwa katika bara la Afrika, licha ya kuwa idadi hiyo bado ni ndogo tukiilinganisha na miradi kama hiyo inayoendelezwa katika mataifa ya Asia na Amerika ya Latina. Miradi hii inajumlisha sehemu ya Mifumo ya Maendeleo Safi (CDM) ya Mkataba wa Kyoto, inayohusikana na mipango mbalimbali ya kuhifadhi mazingira, kuanzia ile miradi ya nishati zinazotumiwa mara kwa mara hadi ile ya kupandisha miti. Miradi kama hii imezisaidia nchi zenye maendeleo ya viwanda kudhibiti vyema matatizo ya hewa chafu na kupunguza halijoto katika dunia, baada ya kuamua pia kuwekeza kwenye miradi ya kupunguza utoaji wa hewa chafu katika nchi zinazoendelea. Miradi 112 ya CDM, inayogharamiwa Yuro milioni 212 kwa mwaka, inasubiri kuthibitishiwa nchi za Afrika kwa sasa, na inasubiri "usajili rasmi". Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na UNEP, inaonyesha kuwepo ongezeko la kutia moyo katika Afrika tukilinganisha na 2008 ambapo miradi 78 ya kutunza mazingira ilisajiliwa kwa Afrika; wakati katika 2004 ni miradi miwili tu ya CDM ilisajiliwa kwa bara zima la Afrika. Asilimia 80 ya miradi ya sasa inayongojea kutekelezwa katika nchi za Afrika kusini ya Sahara - na hujumlisha miradi 28 itakayotendeka Afrika Kusini, ikifuatiwa na miradi ya CDM 14 kwa Kenya. Kuhusu Afrika Kaskazini, Misri inaandaa miradi 13 ya CDM, ikifuatiwa na Morocco ambayo inajitayarisha kutekeleza miradi 10. Wataalamu wanasema Serikali za Afrika zimedhamiria kihakika kuleta mabadiliko yenye natija za kimazingira wiki chache tu kabla ya Mkutano Mkuu wa UM juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa utakaofanyika Copenhagen kuanzia tarehe 07 mpaka 18 Disemba 2009.

Mazungumzo ya upatanishi juu ya Darfur, yatakayosimamiwa na Mpatanishi Mkuu wa Pamoja wa UM-UA kwa Darfur, Djibril Bassolé yanatazamiwa kuanzsihwa tena Ijumatano ya 18 Novemba (2009) kwenye mji wa Doha - na mara hii mashirika ya kiraia kutoka Darfur vile vile yatajumuishwa kwenye majadiliano haya, wakiwemo wawakilishi wa makundi ya wanawake na vijana. Kutokana na taarifa ya karibuni ya mpatanishi Bassolé hatua ya kuwahusisha makundi ya kiraia kwenye mazungumzo ya amani kwa Darfur ina lengo la kuwapatia sauti ya kuchangisha kwenye utekelezaji wa matokeo ya mpango wa amani wa Doha. Mazungumzo ya Doha, yalifanikiwa kufanyika kwa sababu ya mchango wa Serikali ya Qatar, ulioipatia Serikali ya Sudan pamoja na makundi ya waasi fursa ya kujadiliana na kufikia hatua zitakazosukuma mbele mpango wa amani kwa Darfur.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kujiunga kwenye kampeni kubwa kabisa ya kuchanja mamilioni ya watu katika Afrika Magharibi dhidi ya homa ya manjano. Kampeni hii itaanzishwa rasmi wiki ijayo, na italenga kuchanja watu milioni 12 katika mataifa ya Benin, Liberia na Sierra Leone, nchi tatu zinazokabiliwa na hatari ya miripuko ya maradhi ya homa ya manjano kwenye maeneo yao. Hizi ni operesheni za awali kutekelezwa kimataifa, ambapo uchanjaji wa homa ya manjano unafanyika katika nchi kadha kwa wakati mmoja.

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) linajiandaa kuwasilisha makala maalumu ya ripoti juu ya Hali ya Watoto Duniani kwa 2009, ili kuadhimisha miaka 20 ya Mkataba wa Haki ya Mtoto. Ripoti ya mwaka huu itazingatia namna Mkataba ulivyoathiri maisha ya mamilioni ya watoto duniani, na vizingiti wanavyokabiliwa navyo katika kuimarisha maendeleo yao. Mkataba wa Haki za Mtoto ni chombo cha awali cha sheria ya kulazimisha kimataifa, yenye kuthibitisha kidhati haki za binadamu kwa watoto wote ulimwennguni. Mkataba huu unakaribia sasa kuthibitishiwa na takriban Mataifa Wanachama yote, baada ya kuridhiwa na washiriki husika kuanzia 1989. Mnamo Ijumaa ya tarehe 20 Novemba kutafanyika taadhima maalumu za ukumbusho wa Miaka 20 ya Mktaba wa Haki ya Mtoto kwenye ukmbi wa Baraza la Udhamini katika Makao Mkuu ya UM ya jiji la New York.

Imetangazwa leo na Ofisi ya Msemaji wa KM juu ya kuteuliwa kwa Martin Nesirky, raia wa Uingereza kuwa Msemaji mpya wa KM Ban Ki-moon, atakayemrithi Michele Montas, kutoka Haiti ambaye anatazamiwa kustaafu mwisho wa Novemba. KM alinakiliwa akitoa shukrani za dhati kwa bidii ya kazi na mchango wa Bi. Montas ambaye alikuwa Msemaji wake tangu alipojiunga na UM tarehe 01 Januari 2007. Taarifa ilisema Nesirky anajumlisha uzoefu wa miaka 20 ya uandishi habari, na kwenye uhusianao na vyombo vya habari pamoja na kwenye masuala yanayofungamana na uhusiano wa kimataifa. Ataanza kazi na UM kutokea Shirika la Ulaya juu ya Usalama na Ushirikiano (OSCE) lenye makao yake Vienna, Austria, taasisi ambayo Nesirky aliitumikia kwa miaka mitatu ziada kama Msemaji wake na Mkuu wa Vyombo vya Habari na Mawasiliano ya Umma.